Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma.

Serikali imesema takwimu Duniani zinaonesha kuwa ushiriki wa wanawake na wasichana katika elimu na ajira kwa fani za sayansi ni mdogo ikilinganishwa na ushiriki wa wanaume katika fani hiyo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga amesema hayo Februari 7,2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya kitaifa ya siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi ambayo huadhimishwa Fruari, 11 kila mwaka.

Amesema hali hiyo inapunguza juhudi za kufikia usawa wa kijinsia katika elimu na ajira hivyo kuahidi kushughulikia changamoto hiyo kuleta usawa.

Kutokana na hali hiyo ameeleza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa kushirikiana na wadau katika sekta ya umma na binafsi, imeandaa maadhimisho haya ili kuwachochea wanawake kuongeza bidii kwenye masomo hayo.

“Kwa mwaka huu 2025, hafla ya Kitaifa ya kuadhimisha siku hiyo itafanyika siku ya Jumanne tarehe 11, Februari, katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), Jijini Dodoma, na Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Prof. Adolf Mkenda,”amesema.

Amesema Tanzania inatambua usawa wa kijinsia ni muhimu kwa kufikia malengo ya maendeleo yaliyokubaliwa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, kutokana na maazimio hayo ya Umoja wa mataifa, Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi kuanzia mwaka 2021.

“Lengo la kuadhimisha siku hii, ni kutambua na kusherehekea mchango wa wanawake na wasichana katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), maadhimisho haya ni fursa ya kuhamasisha wanawake na wasichana zaidi kujiunga katika nyanja hizi ili kubadili mustakabali wao na jamii zetu kwa ujumla, “ameeleza na kuongeza kuwa,

Masuala ya wanawake na wasichana ni mtambuka na hivyo yanahitaji ushiriki na mchango wa wadau wote bila kujali wako katika sekta ya umma au binafsi,”amesema.

Waziri Kipanga ameongeza kuwa kupitia maadhimisho ya mwaka huu wanaendelea kuhimiza juhudi mbalimbali zinazokusudiwa katika kuimarisha uelewa wa watanzania kuhusu umuhimu wa kushirikisha wanawake na wasichana katika uongozi na maamuzi juu ya masuala ya sayansi.

Amesema wanahitaji kuhamasisha kizazi kilichopo na kijacho cha wasichana kupenda na kujiunga na masomo ya sayansi kwa kuondoa dhana potofu na kutoa fursa sawa katika elimu na maendeleo ya kitaaluma.

Amesema ,”Wazazi, walimu, viongozi wa dini na kijamii, na wadau wote tuna wajibu wa kuhakikisha wasichana wanapata elimu bora na fursa sawa za kujihusisha na nyanja hizi, hivyo kwa pamoja wanaweza kubadili mustakabali wa taifa kwa kuhakikisha wanawake na wasichana wanachangia kikamilifu katika maendeleo ya sayansi na teknolojia.), “amesisitiza

Mwishoo