Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini agizo linalozuia wanawake waliobadili jinsia kushindana katika michezo ya wanawake.
“Kuanzia sasa, michezo ya wanawake itakuwa ya wanawake tu,” Trump alisema, akizungukwa na wanariadha wanawake na wasichana kabla ya kusaini agizo hilo huko White House. “Kwa agizo hili, vita juu ya michezo ya wanawake imekwisha.”
Kulingana na yeye, Marekani itakataza visa wanamichezo waliobadili jinsia.
Agizo hilo ambalo linaanza kutumika mara moja linatoa mwongozo, kanuni na tafsiri za kisheria, na litaorodhesha Idara ya Elimu kuchunguza shule za upili zinazodhaniwa kutofuata sheria.
Warepublican wanasema hatua hiyo inarejesha usawa katika michezo lakini wanaotetea haki za LGBT na mashirika ya haki za binadamu yameielezea kama ya kibaguzi.
Afisa wa utawala alisema kuwa agizo hilo litabadilisha msimamo wa utawala wa Biden ambao mnamo mwezi Aprili mwaka jana ulisema kwamba wanafunzi wa LGBT watalindwa na sheria ya shirikisho, ingawa haikutoa mwongozo maalum kwa wanariadha waliobadilisha jinsia.
Rais Trump alibainisha kuwa agizo hilo litajumuisha Michezo ya Olimpiki ya 2028 huko Los Angeles.
Siku ya kwanza ya Trump madarakani tarehe 20 Januari, alitia saini agizo tofauti akitaka serikali ya shirikisho ifafanue rasmi jinsia kuwa ni mwanamume au mwanamke.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/image-14.png)