Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kimeendesha mafunzo jumuishi kwa vitendo kwa wanafunzi wa Astashahada na Stashada, kuonesha kwa vitendo kile walichojifunza katika muhula wa kwanza wa masomo.

Akizungumza katika hafla fupi wakati wa mafunzo hayo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Taaluma, Tafiti na Ushauri Bi. Jesca William amesema mafunzo kwa vitendo ni muhimu kwani yanakwenda kuwaimarisha wanafunzi na kupata ujuzi itakaowawezesha kumudu soko la ajira mara wamalizapo masomo yao.

‘Kwa tukio hili wanafunzi wanatuhakikishia kwamba wako tayari kuingia kwenye soko la ajira. Sisi ni Chuo kinachojikita kwenye videndo ili mwanafunzi akimaliza aweze kumudu shindani kwenye soko la ajira ndani na nje ya nchi sabamba na kujiajiri wenyewe’ amesema Jesca.

Aidha, amewapongeza walimu kwa kujitoa kwao katika kuhakikisha wanafunzi wote wanapata mafunzo stahiki kwa nadharia na vitendo, na kuwataka wanafunzi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Taaluma wa Chuo hicho Claudia Nshekanabo amesema mafunzo hayo yanakwenda kuwapima wanafunzi kwa vitendo kutoa huduma zote kwa namna walivyooelewa wakiwa darasani.

Amesema mafunzo hayo yamehusisha Idara ya uratibu wa matukio na ukarimu zinazotoa huduma kwa wageni na watalii, ikiwemo vyakula, vinywaji, malazi na uratibu wa matukio.

‘Mafunzo haya yamehusisha wanafunzi 30 wa Astashahada na Stashada. kutoka muhula wa kwanza wa masomo na yanafanyika kila muhula mpya napokaribia kumalizika kabla ya kuingia kwenye mitihani’ amesema Bi. Nshekanabo.

Naye Dorothea Gangai mwanafunzi wa mwaka wa pili katika sanaa ya upishi amewashukuru walimu wa Chuo hicho kwa kuwajengea uwezo, ambapo wamekuwa mahili katika fani mbalimbali hata kabla muda wa kuhitimu masomo yao haujafika.

‘Tunawashukuru sana walimu wetu, wanakufundisha mpaka unaelewa, hapa hata kama utakuja na uelewa mdogo, utaondoka na ujuzi tu, walimu wanatoa ushirikiano wa hali ya juu sana” amesema Gangai.

Chuo cha NCT kinaendeesha mafunzo hayo kila wanapomaliza muhula wa masomo kwa lengo la kuwapima wanafunzi wao kuelekea katika ratiba ya mtihani.