Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeelezea hatua ya kusitishwa mapigano iliyotangazwa na waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo kama “mawasiliano ya uongo.”

Kulingana na msemaji wa serikali ya Kongo Patrick Muyaya, wanachosubiri kwa sasa ni kuondoka nchini humo kwa waasi wa M23.

Kongo imesema hayo wakati ambapo Umoja wa Mataifa umeripoti mapigano makali kati ya M23 na jeshi la Kongo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari kuwa wamepokea ripoti za mapigano Kivu Kusini ingawa hawana taarifa zozote za M23 kuukaribia mji wa Bukavu.

Wataalam wa Umoja wa Mataifa wanasema M23 wanaungwa mkono na kikosi cha wanajeshi 4,000 wa Rwanda.

Idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na mwaka 2012 pale waasi hao walipouteka mji wa Goma kwa muda kisha wakaondoka baada ya shinikizo la kimataifa.