Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia l, Arusha
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) leo imeendesha semina juu ya ujumuishaji wa masuala ya jinsia katika utoaji wa fidia huku kundi la wanawake likitajwa kuathiriwa zaidi na ukiukaji wa haki za binadamu barani Afrika.
Jaji wa Mahakama hiyo Jaji Imani Daud Aboud amesema semina hiyo inalenga kujadili Kaulimbiu inayosema “Kutoa Haki kwa Wanawake Kupitia Fidia” kwani haki za wanawake zimekuwa zikivunjwa zaidi kuliko makundi mengine ndani ya Jamii.
Amesema haki za wanawake zimeendelea kuvunjwa barani Afrika na duniani kwa ujumla katika maeneo mbalimbali kama vile majumbani, makazini na katika maeneo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
“Wanawake wamekuwa wakikumbwa na unyanyasaji wa kingono, kijinsia na unyanyasaji mwingine……. mjadala wa leo umejikita katika kubadilisha fikra zetu kuanzia serikalini na katika vyombo vya haki ili kubadilisha mitazamo yetu juu ya haki za wanawake ili wapate haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kuheshimika”
Amesema ukiukaji wa haki za wanawake unatokana na misingi na tamaduni zilizopo ambazo zinapaswa kubadilishwa ili ziweze kulinda haki za kundi hilo.
“Tunapozungumzia suala la fidia watu wengi wanahisi ni fidia ya fedha, sasa tujiulize je fidia ya pesa inatosha? jibu ni hapana kwani wanawake hawahitaji fidia ya pesa bali wanahitaji kuheshimika na kupata haki zao za msingi kama vile huduma bora za afya, ulinzi na elimu kupitia misingi ya uongozi imara wa nchi zetu” alifafanua Jaji Imani.
Washiriki wa semina hiyo walijadili juu ya udhalimu wa kihistoria na ukiukaji wa kimfumo unaoathiri wanawake na wasichana, jinsi ukiukaji wa haki za binadamu unavyoweza kuathiri wanawake na wanaume kwa njia tofauti na hitaji la ujumuishaji wa masuala ya kijinsia katika utoaji wa fidia mjadala ambao uliibuliwa na Mtaalam mbobezi wa sheria katika eneo la utoaji wa fidia Profesa Joy Ngozi Ezeilo.
Mada nyingine iliyojadiliwa ni fidia kwa ajili ya ukiukaji wa haki za binadamu unaoathiri makundi tofauti ya wanawake wakiwemo wanawake kutoka jamii za wazawa, wanawake walioathiriwa na ukatili wa kingono na kijinsia, wanawake wenye ulemavu, wanawake waliokimbia makazi yao ndani ya nchi pamoja na wanawake wazee na wajane.
Semina hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, Majaji wa Mahakama wa Afrika, Majaji kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Mabalozi, wadau kutoka vyuo vikuu pamoja na wadau kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania.