Wiki iliyopita nchi hii ilitawaliwa na mjadala wa uamuzi wa Serikali kurejesha viboko shuleni. Mjadala huu najua umegusa mifano mingi. Wachangiaji wengi wamerejea vitabu vya imani mbalimbali, vinavyoeleza jinsi fimbo inavyosaidia kumnyoosha mtoto.

Mimi sitarejea kwenye vitabu vitakatifu, maana naamini nitakuwa siongezi wala kupunguza chochote katika yaliyokwishasemwa hadi sasa. Niseme mapema tu kwamba bila fimbo, elimu tutaisikia kwenye viota vya ndege.


Sitanii, nchi nyingi zimejaribu kufuta viboko shuleni, ikiwamo Uingereza, lakini kwa sasa wameamua kurejesha viboko shuleni. Tatizo tulilonalo kama nchi ni kudhani Wazungu wanajua kila kitu. Wamezigeuza nchi zetu kuwa gunia la mazoezi ya mawazo yao potofu.

 

Wamekuja na wazo kuwa viboko vifutwe shuleni, na kutokana na misaada uchwara wanayotupatia isiyotuondoa katika lindi la umasikini zaidi ya kujidhalilisha kama nchi, tunakubali. Tumekubali vikajitokeza vi-NGO uchwara pia vikapiga tarumbeta.

 

Sitanii, nakumbuka wakati tuko shule, tulikuwa na mwalimu anatufundisha Kiingereza akijulikana kwa jina la Marcel Rweyemamu. Mwalimu huyu tukiwa katika elimu ya msingi, ukikosea ‘spelling’ katika kila neno anakuandikia “SP” na mwisho wa kazi uliyoifanya anakuandikia “see me”. Hadi tunamaliza darasa la saba, Mwalimu Marcel tulikuwa tunamwita “see me”. Ukienda kumwona Mwalimu Marcel, hakuwa akikushirikisha kikombe cha chai au kukupa simu yake utume meseji. Sisi ilikuwa huwezi kumkumbatia mwalimu wako (ila siku hizi inawezekana), bali anakupatia alichokuwa akikiita “chapati kutoka kwa Kapesa.”


Chapati hizi wala si chapati kama wengi mnavyodhani, hapo shule ya Msingi Kyakailabwa, Bukoba ofisi ya walimu, ilikuwa na sakafu murua. Anachora mduara na kukwambia usimame katikati ya mduara ule. Kisha anatafuta fimbo zinazonesanesa. Anakuchapa viboko kwenye vifundo vya miguu sawa na idadi ya maneno uliyoyakosea.

 

Kama umekosea 50, utacharazwa fimbo 50. Hadi tunamaliza darasa la saba, kwa hofu ya fimbo za Mwalimu “see me” hata wale ambao hawakuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari, leo nikikutana nao wanazungumza Kiingereza kuliko baadhi ya wahitimu wa chuo kikuu.


Miaka 20 iliyopita nikiwa nafundisha katika Shule ya Sekondari ya Mugeza huko Bukoba, darasa langu la kwanza la Kidato cha Tatu, walikuwa ni wale wanafunzi wa msamaha wa Mwinyi, kama mnawakumbuka.


Sitanii, wanafunzi wa kidato cha pili mwaka 1993 walishindwa mtihani kwa kiwango cha kutisha na Rais Ali Hassan Mwinyi akaamuru kiwango cha ufaulu kwenda kidato cha tatu kishushwe hadi alama 14, badala ya 21. Hili ndilo darasa nililolipokea kulifundisha.

 

Nilipofika Sekondari ys Muheza nilikuta kijiwe wanakiita JB (Jobless). Niliwashawishi wasiende JB wanafunzi wakaniona kama chizi. Wakati huo nikiwa nimetoka JKT ninayo mafunzo ya kijeshi, nikaamua kuwapeleka kijeshi.

 

Kidato cha tatu nilikuwa nafundisha somo la Kiingereza na katika vitabu vya fasihi nikafundisha kitabu cha “Things Fall Apart” kilichoandikwa na Chinua Achebe. Mhusika Mkuu alikuwa Okonkwo. Nilidadavua kitabu kile, nikamweleza kijana Unoka na katika Kijiji cha Umuofia walivyomwogopa Okonkwo.

 

Hadi naacha kazi Sekondari ya Mugeza na kujiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari Nyegezi, Mwanza, wanafunzi karibu wote shuleni hapo walikuwa wakiniita Okonkwo. Hakika kama ni fimbo nilizitembeza. Ingekuwa leo ningekuwa gerezani. Wale wanafunzi wa msamaha wa Mwinyi wakafanya maajabu katika mitihani ya kidato cha nne.


Leo ninavyoandika makala haya, darasa hilo linao mawakili kadhaa, maafisa utumishi, watendaji katika kampuni mbalimbali na kila nikikutana nao tunakumbusha (kwa utani) fimbo za Mugeza Sekondari. Napata faraja kukutana na wanafunzi wangu wakiwa mawakili na vyeo vikubwa katika kampuni mbalimbali.


Sitanii, nafarijika zaidi wanaponiambia kuwa jinsi nilivyowabana (kwa fimbo) ndivyo walivyosoma zaidi na hatimaye kushinda mitihani yao. Narudia, si kwamba sikuwapenda watoto hawa, bali kwa umri wao walihitaji mwongozo. Mwongozo ukiendana na fimbo katika umri mdogo, basi japo kwa hofu mafundisho yanashikika vichwani mwao.

 

Nasema ushauri wa Wazungu kututaka tufute viboko kwa watoto wetu, uliona mbali. Walijua tutajenga taifa la mazezeta na wataendelea kututawala tukiwa hapa kwetu. Sasa tumefanikiwa kushituka, ni wajibu wetu kuchagua kama tuendelee kuwaahidi watoto mayai na biskuti waharibike au tuwachape fimbo wajenge familia zao na taifa letu siku za usoni.