Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha
Rais wa Jamhuri ya Cape Verde, José Maria Neves, amesema nchi za Afrika zinaweza kuongoza mabadiliko ya maisha yao ya baadaye kwa kuondokana na utegemezi wa ukoloni mamboleo kwa kudai fidia iliyotokana na dhuluma za kihistoria na kimfumo.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mwaka wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) Jiji Arusha, Rais Neves amesema mahakama hiyo inaashiria kujitolea kwa Bara la Afrika kwa haki na upatanisho lakini ni lazima iwe kamili kwa kupewa rasilimali.
Aidha amesema ni wakati sasa nchi za Afrika kurejeshewa utu uliovunjwa na kuhakikisha kuwa uhalifu huo haujirudii tena kwa kujenga mazingira ya kuponya majeraha pamoja na kuhakikisha kunakuwepo heshima na haki sawa kwani bila haki hakuna amani ya kudumu na bila amani hakuna maendeleo.
Amesema suala la fidia kwa Afrika itasaidia kuponya majeraha yaliyotokana na biashara katili ya utumwa ambapo jasho la Waafrika lilitumika kulisha uchumi wa mataifa mengine.
“Sasa ni wakati wa kuchukua hatua, fidia kwa njia ya haki inamaanisha kutambua mateso ya waadhiriwa, kurejesha utu wao uliovunjwa na kuhakikisha kuwa uhalifu uliofanywa haurudii tena kwa kujenga mazingira ambapo majeraha yaliyopita yanaweza kupona, kwani bila haki, hakuna amani ya kudumu na bila amani hakuna maendeleo ” alisema Rais Neves.
Amefafanua kuwa fidia katika utamaduni siyo kujenga upya majengo au fidia kwa hasara ya nyenzo bali ni kurejesha mila zilizosahaulika, kurudisha ubinadamu kwa Afrika, kuhakikisha kwamba ngoma za amani zinavuma kuliko tarumbeta za vita.
“….. inamaanisha kujenga mustakabali ambapo misemo ya kitamaduni ya kiafrika inahamasisha ulimwengu na kila mwafrika anaweza kujivunia urithi wake, hivyo ni juu yetu kwamba ahadi hii inatekelezwa ili kuuambia ulimwengu kuwa tunaweza kuokoa utu na kurekebisha dhulma na uadui……”
Amesema Bara la Afrika ni tajiri kwa hadithi, nyimbo, ngoma na ishara ambazo zimeunda utambulisho wake wa karne lakini migogoro ya kihistoria umeumiza urithi huu kwa kupora maeneo, lugha zetu kunyamazishwa na maarifa ya mababu zetu kusahaulika.
Akisoma risala ya ufunguzi, Rais wa Mahakama hiyo Jaji Imani Daud Aboud amesema mwaka huu wa Mahakama umekuja na mada yenye ujumbe wa “Kuendeleza Haki kwa njia ya Fidia” pamoja na Kaulimbiu ya “Haki kwa Waafrika na Watu Wenye Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia” ambayo inaangazia kwa kina historia ya Afrika, mapambano yanayoendelea kwa ajili ya haki pamoja na na matarajio ya siku zijazo.
Amesema Mahakama ya Afrika imechagua mada hiyo kwa makusudi na kwa wakati muafaka kwani makovu yatokanayo na historia ya utumwa, ukoloni, ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kimfumo pamoja na unyonyaji wa kiuchumi unaendelea kuonekana katika bara la Afrika na kusisitiza kuwa udhalimu huu siyo wa kuachwa kama zamani.
“Fidia ni zaidi ya fedha, ni njia muhimu ya kushughulikia maadili na madeni ya kiuchumi yaliyotokana na dhuluma za kihistoria na kimfumo, fidia itasaida kuponya majeraha makubwa ya siku za nyuma huku zikitoa dhamana kwamba ukatili hautarudiwa tena” amesema Jaji Imani.
Akisisitiza juu ya suala la fidia kwa Afrika Jaji Mkuu wa Mahakama hiyo Bheki M. Maphalala amesema suala hilo si jambo la hivi karibuni kwani hata kwenye Tangazo la Abuja la 1993 limepata nguvu na kupitia mipango iliyofuata kama vile Azimio la Durban la 2001 na Tangazo la hivi karibuni la Accra la 2023 kuhusu fidia ni miongoni mwa juhudi zinazosisitiza haja kubwa ya kushughulikia matokeo ya kudumu ya utumwa, ukoloni, ubaguzi wa rangi na aina nyinginezo za ubaguzi.