Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mwenyekiti Bodi ya Uongozi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Dkt. Richard Masika amekiri kuridhishwa na hatua zinazofanywa na Tume katika utekelezaji miradi ya Umwagiliaji ikiwemo mradi wa ujenzi bwawa la
Umwagiliaji Membe lililopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Dkt. Masika ametoa kauli hiyo mara baada ya kufanya ziara katika bwawa hilo ambapo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 86 ya utekelezaji wa mradi.

Aidha Dkt. Masika ametoa wito kwa wakulima ambao ni wanufaika wa mradi huo kutoa ushirikiano kwa wataalamu wanaotekeleza mradi wakati wa ujenzi na mara baada ya kukamilika kwake ili kuhakikisha unaleta tija kwa wakulima.

Sanjari na hayo Dkt. Masika ameielekeza Tume kuhakikisha katika utekelezaji wa mradi huo izingatie muda na thamani ya mradi iendane na utekelezaji.

Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkurugenzi Idara ya Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini Dkt. Consolatha Kapinga amekiri kupokea maelekezo ya Mwenyekiti huyo wa Bodi na kuahidi kuwa Tume itahakikisha inayafanyia kazi.

“Kati ya maelekezo hayo muhimu ni pamoja na Tume kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili kuleta manufaa kwa wananchi wa Dodoma na Taifa kwa ujumla, hivyo tutahakikisha hilo linatekelezwa,”amesema.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wanufaika wa mradi huo Kaimu Mwenyekiti wa kijiji cha Membe Samweli Malima, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuhakikisha mradi unakamilika kwani utachangia kukuza kipato cha wakulima, hasa kundi la vijana anbao watajishughilisha na kilimo.

Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Membe, unaotekelezwa na mkandarasi NAKUROI INVESTMENT CO. LTD, umefikia asilimia 86 ya utekelezaji.

Bwawa hilo lenye thamani ya Shilingi bilioni 16.26 litawanufaisha wakulima 1,500 katika eneo la hekta 2,500. Miongoni mwa kazi zilizokamilika ni ujenzi wa tuta la bwawa (84%), ukuta wa zege (87%) na mfumo wa kutolea maji (92%).

Katika hatua nyingine, mradi wa skimu ya
Umwagiliaji Membe unaotekelezwa na mkandarasi CRJE EAST AFRICA LTD umefikia asilimia 25.5 ya utekelezaji wake. Mradi huu wenye thamani ya Shilingi bilioni 19.39 unatarajiwa kunufaisha wakulima 1500. katika eneo la hekta 2,500.

Hata hivyo, baadhi ya kazi kama ujenzi wa mifereji ya kutolea maji mashambani bado hazijaanza.

Sambamba na miradi ya umwagiliaji, Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 75 katika skimu ya Membe, mradi huo wa Shilingi bilioni 6.69 unaendelea kwa kasi, ambapo misingi ya nyumba 67 imekamilika, huku nyumba 8 zikiendelea na maandalizi ya umwagaji wa zege.