Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga
Watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Tanga na Pwani wametakiwa kufanya kazi kwa weledi, bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hilo.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Rufaa Jacobs Mwambegele ametoa wito huo jijini Tanga, mkoani Tanga leo Februari 02, 2025 wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa daftari ngazi ya mkoa, mkoani humo.
“Baadhi yenu mlibahatika kushiriki katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Tume ikiwemo uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika awamu zilizopita. Kwa kutumia uzoefu mlionao na mafunzo mtakayopatiwa, ninaamini mtafanya kazi zenu kwa weledi, bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hili,” Jaji Mwambegele amewaambia watendaji hao.
Amewataka kutumia uzoefu walionao kuwasaidia wenzao ambao hawakuwahi kushiriki katika zoezi kama hilo ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Akifungua mafunzo kama hayo Mkoani Pwani, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk amewaasa watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji.
“Ni muhimu kutekeleza majukumu yenu kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji hasa ikizingatiwa kuwa, vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini,” amesema Jaji Mbarouk.
Ameongeza kuwa kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivyo kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hilo muhimu, na kwamba wana wajibu wa kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili waweze kuyafanyia kazi wakati zoezi hilo la uboreshaji wa daftari litakapokuwa limeanza kwenye maeneo yao.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika mkoani Tanga na Pwani kwa siku saba kuanzia tarehe 13 hadi 19 Februari, 2025 ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa saa 02:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Zoezi hilo ambalo lilizinduliwa mkoani Kigoma mwezi Julai, 2024 limeshakamilika kwenye mikoa 25 ambayo ni Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma, Singida, Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe, Njombe na Ruvuma.