Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeanza maandalizi ya mzunguko wa 11 kati ya mizunguko 13 ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mikoa ya Pwani na Tanga ambayo zoezi la uboreshaji litaanza Februari 13 hadi 19, 2025.

Tume inaendelea na zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambapo uzinduzi wa awali ulifanyika mkoani Kigoma Julai 20, 2024, na ulianzia katika mikoa ya Kigoma, Tabora, na Katavi.

Akifungua mkutano wa Tume ya Uchaguzi Mkoani Pwani, Jaji (Rufaa) Mbarouk Mbarouk, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, alisema hadi Januari 16, 2025, Tume hiyo imekamilisha uboreshaji wa daftari katika mikoa 25, ikiwa ni pamoja na mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora, na Katavi.

“Kwa sasa, mikoa miwili ya Mtwara na Lindi, pamoja na sehemu ya mkoa wa Rukwa, katika Halmashauri za Madaba, Namtumbo, na Tunduru, inatarajiwa kukamilisha zoezi hili ifikapo Februari 3, 2025,” aliongeza.

Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Suleiman Mtibora, alieleza kuwa Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya milioni 5.586.433, huku watakaobadilisha taarifa zao wakitarajiwa kuwa milioni 4.3.

“Katika mkoa wa Pwani, wapiga kura wapya wanatarajiwa kuwa 186,211, sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 992,067 waliopo kwenye daftari la wapiga kura, baada ya uandikishaji, mkoa huo utakuwa na wapiga kura milioni 1.178,278,” aliongeza Mtibora.

Aidha, alieleza kuwa watu 534,000 wanatarajiwa kutolewa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kutokana na kukosa sifa, ikiwa ni pamoja na vifo, kutokuwa na akili timamu, na wale wanaotumikia kifungo kwa zaidi ya miezi sita.

Mtibora alibainisha kwamba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia kuwa na jumla ya wapiga kura milioni 34.7.

Kuhusu vituo vya uandikishaji, alisema kuwa Tanzania Bara vitakuwa vituo 29,753, na visiwani Zanzibar 417, jumla ya vituo ikiwa 40,170.

Kwa upande wa mkoa wa Pwani, kutakuwa na jumla ya vituo 1,913 vya kujiandikisha, ikiwa ni ongezeko la vituo 179 kutoka 1,734 vilivyokuwepo mwaka 2019/2020.

Kadhalika, alisema kuwa kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 114(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024.

Aliwaasa wananchi kuacha kujiandikisha zaidi ya mara moja kwani atakayebainika akikiuka agizo hilo atakutana na adhabu ya faini isiyopungua laki moja na isiyozidi laki tatu, au kutumikia kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili, au vyote kwa pamoja.

Aliwahimiza wananchi kujitokeza kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kufanikisha zoezi la kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba.

Mkurugenzi Msaidizi wa Daftari na TEHAMA, Martine Mnyenyelwa, alielezea kuwa katika uboreshaji huu, kama ilivyokuwa kwa miaka ya 2015-2020, kutatumika teknolojia ya Biometric Voter Registration (BVR).

Hata hivyo, tofauti na uandikishaji wa mwaka 2015 na uboreshaji wa mwaka 2020, uboreshaji wa mwaka 2024/2025 utatumia BVR kits zilizoboreshwa kwa kutumia programu endeshi ya kisasa zaidi.

Mnyenyelwa alisema, BVR kits zitakazotumika zimepunguzwa uzito ambapo zitakuwa rahisi kubebeka na kufanya zoezi la uboreshaji kuwa rahisi haswa kwenye maeneo ya Vijijini ambako watendaji hulazimika kubeba vifaa kwa umbali mrefu.

“Tume katika kuhakikisha inaenda na mabadiliko ya teknolojia ikiwa ni sanjali na kurahisisha zoezi hili imeboresha mfumo wa uandikishaji ambao kwa mara ya kwanza utamuwezesha mpiga kura aliyepo kwenye daftari kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zake au kuhama kituo kwa kutumia aina yoyote ya simu ya kiganjani ama kompyuta”