Mkutano umejiri baada ya wanajeshi 13 kutoka Afrika Kusini na watatu kutoka Malawi, kuuawa katika mapigano Goma nchini DRC, ambapo walikuwa wamepelekwa kama sehemu ya juhudi za kudumisha amani za kikanda.

Viongozi wa mataifa ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wametangaza uungaji mkono thabiti kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, katika mapambano yake dhidi ya waasi wa M23 waliosaidiwa na Rwanda kuuteka mji wa Goma.

SADC ilifanya mkutano wa dharura nchini Zimbabwe kuhusu mzozo unaoendelea mashariki mwa Kongo, ambao umeibua wasiwasi kuhusu usalama wa kikanda. Kongo ni moja ya nchi 16 wanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda.

Mkutano huo ulifanyika baada ya wanajeshi 16 kutoka Afrika Kusini na Malawi, pia wanachama wa SADC, kuuawa katika mapigano ya karibuni karibu na Goma, ambako walikuwa wamepelekwa kama sehemu ya juhudi za kudumisha amani.

Mkutano huo umesema malengo ya operesheni za kudumisha amani zilizozinduliwa Desemba 2023 “bado hayajatimizwa,” na kutoa wito wa kutumwa kwa maafisa wa ulinzi  kutoka nchi zenye wanajeshi katika kikosi cha amani ili kufanya tathmini ya wanajeshi waliopo katika eneo hilo.

Mbali na Afrika Kusini na Malawi, Tanzania pia ina wanajeshi katika kikosi hicho. Taarifa hiyo ilithibitisha pia wito wa kuitishwa kwa mkutano wa pamoja wa SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki “kutathmini hali ya usalama nchini Kongo na kujadili mkakati wa kusonga mbele.