Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Chato
WANANCHI wilayani Chato mkoani Geita wamejitokeza kumchangia Rais Samia Suluhu Hassan kiasi cha Sh milioni 1.4 kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uraisi katika uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Mchango huo umefanyika katika hafla maalum iliyoandaliwa na Kamati ya Amani ya Wilaya ya Chato inayoundwa na viongozi wa dini mbalimbali kwa ajili ya kuliombea taifa dhidi ya ugonjwa wa Marburg.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Serikali ya Tanzania ilithibitisha kuwepo kwa ugonjwa wa Murburg wilayani Biharamulo mkoani Kagera ambapo ni jirani na Chato.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya wilaya, Sheikh Abdalah Aman Isimail amesema hatua hiyo ni ishara ya wanachato kumpenda Rais Dk Samia Suluhu pamoja na mapenzi kwa taifa lao.
Amesema mbali na kuliombea taifa wao kama kamati ya amani ya wilaya wameruhusu jambo hilo lifanyike kama ishara ya kurejesha fadhila kwa mema aliyoyatenda Rais Dk Samia tangu achukue madaraka mwaka 2021.
“Tendo hili mlilolifanya wananchi wa Chato bila nguvu yeyote Mungu mwenyewe ametuongoza tukapata kiasi hiki, mkuu wa wilaya alisema fomu ni milioni moja, ila sisi tayari tumeipata pesa ya mama Samia kuchukua fomu ya urais.
“Kwa hiyo huko asijitokeze mwingine anataka kumchukulua mama fomu, wanaChato tumechanga pesa ya kutosha mama Samia kuchukua fomu kwenye maombi ya kuiombea nchi wanachato tumeshachanga.
Hii ni dhamana ya wanachato, hii ni amana ya wanachato, haya ni mapenzi ya wanachato. Na salamu za Chato zitafika, wanachato kwa mapenzi yao wamesema kwamba asitafute hela ya kwenda kutafuta fomu’, amesema.
Katibu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania CPCT Geita, Joshua Wiliam amesema dhamira ya kuliombea taifa na viongozi wake ni kuhakikisha Tanzania inaendelea kutawaliwa na viongozi wake kwa amani na usalama.
Mkuu wa wilaya ya Chato, Louis Bura amewapongeza wakazi wa Chato kwa uamuzi wa kuliombea taifa, viongozi na kumchangia Rais Dk Samia pesa ya kuchukua fomu kwani ni uamuzi unaowapa moyo viongozi wa nchi.
“Na mimi kama Kamisaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), niwashukuru sana kwa hafla hii, wazo hili limetoka kwenu nyinyi wana Chato, ingekuwa limetoka kwangu mimi mkuu wa wilaya ingekuwa kama nalazimisha jambo fulani.
“Kwa kuwa mmeamua nyinyi wenyewe kwa mapenzi yenu mliyonayo, mimi nawashukuru sana na ishara salamu hizi zitamfikia mama Samia, Mungu awabariki sana na awaongezee pale mlipotoa”, amesema.