Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia
Dar es Salaam
TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 19 wa Mwaka wa Jukwaa la Korosho Afrika 2025 wenye lengo la kuonesha fursa za uwekezaji zilizoko kwenye Tasnia ya Korosho kuanzia shambani hadi sokoni.
Ameyasema Januari 31, 2025 Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred Wakati wa Uzinduzi wa Mkutano huo utashirikisha wadau mbalimbali kutoka nchi ambazo ni walaji wa korosho ikiwa ni pamoja na Marekani, Nchi za Ulaya, China, Uarabuni, Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini na nchi zingine za bara la Afrika. na unatarajiwa kufanyika Novemba 18 hadi 22 jijini Dar es Salaam ukumbi wa Julius Kambarage Nyerere JNCC
“Kupitia Mkutano huu tunategemea kupata uwekezaji kwenye mashamba makubwa ya korosho, kuongeza kasi ubanguaji korosho ambapo matarajio ni kuongezeka kwa viwanda vya kubangua na kusindika bidhaa hiyo na kuimarisha masoko kwa kufungua ndani na nje ya nchi za Afrika,” amesema Alfred na kuongeza.
“Naomba kuwashukuru African Cashew Alliance (ACA) kwa maamuzi yake ya kuridhia Mkutano wa 19 wa mwaka 2025 kufanyika nchini Tanzania ikiwa ni mara ya tatu ambapo mara ya kwanza ulifanyika mwaka 2007 na mara ya pili 2019. Mkutano huu hufanyika kila mwaka ambapo kwa mwaka 2024 ulifanyika nchini Benin,”.
Mkutano huo utaongonzwa na wazo kuu “kufungua fursa za uwekezaji kwenye tasnia ya Korosho kwa ukuaji wa uchumi endelevu (Unlocking Cashew Investment Opportunities for Sustainable Economic Growth) huku kauli mbiu ikiwa ni “Wekeza kwenye Korosho kwa Maendeleo endelevu (Invest in cashew for Sustainable Development).
Wazo kuu na kauli mbiu vinaendana na malengo ya Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayokusudia kuuza korosho zilizoongezwa thamani badala ya kuendelea kuuza korosho ghafi.
Kwamba Mkutano huo utatumika kuhamasisha matumizi ya korosho na bidhaa zake kama vile mafuta ya ganda la korosho (Cashewnut Shell Liquid – CNSL), sharubati (juice), maziwa ya korosho (cashew milk), mvinyo (wine), nyama ya mabibo (cashew apple meat) na pombe kali.
Alfred ameeleza bidhaa nyingine kama ethanol zinaweza kutumika kwenye maabara za hospitali na shule zetu na hivyo kupanua wigo wa soko la korosho.
Akizungumzia kuhusu juhudi za Serikali kuendeleza zao hilo alifafanua kuwa Serikali ya Awamu ya sita imefanya juhudi kubwa za kuendeleza zao la korosho ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu sasa imekuwa ikitoa pembejeo za korosho kwa wakulima kwa ruzuku ya asilimia 100.
Ametoa mfano katika msimu wa 2024/2025 ambapo ruzuku ya pembejeo ilikuwa shilingi billioni 182 ambapo utoaji wa pembejeo za ruzuku umechagiza kuongezeka kwa uzalishaji kutoka tani 310,000 msimu wa 2023/2024 hadi kufikia tani 410,000 kwa msimu wa 2024/2025 zilizouzwa kupitia minada.
Amesema ukusanyaji wa taarifa za uzalishaji unaendelea kwa kukusanya takwimu za korosho zinazobanguliwa majumbani kwenye vikundi vidogo na watu binafsi pamoja na uzalishaji katika mikoa mipya.
Kwamba hadi mwisho wa msimu makadirio ni kuzalisha jumla ya tani 500,000 katika msimu wa 2024/2025. Ameongeza Aidha bei ya korosho ghafi katika msimu wa 2024/2025 iliimarika na kufikia shilingi 4,195 kwa kilo ikiwa ni bei ya juu kuliko bei zote zilizopatikana kutoka nchi yetu ipate uhuru.
Ameeleza, pamoja na uwepo wa mahitaji makubwa ya korosho ghafi katika soko la dunia, Uamuzi wa Serikali kutumia mfumo wa mauzo wa Soko la Bidhaa (TMX) umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ushindani katika minada na kuchangia katika kuimarika kwa bei.Pamoja na mafanikio hayo lengo la Serikali ni kuzalisha tani 1,000,000 za korosho ghafi ifikapo mwaka 2029/2030.
Alfred amesema katika juhudi za kufikia malengo hayo Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Korosho imeajiri Vijana 500 kupitia mpango wa jenga kesho iliyo bora (Building a Better Tomorrow) ambao wana jukumu la kusaidia katika utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima pamoja na kusimamia shughuli mbalimbali za uendelezaji wa zao katika kata zote zinazolima korosho katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga Vijana hao watapewa pikipiki pamoja na vishikwambi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Aidha, katika kufikia lengo la kubangua korosho zote zinazozalishwa hapa nchini ifikapo mwaka 2029/2030, Serikali imetenga eneo la ekari 1,572 kwa ajili mradi wa kongani la viwanda lililopo kijiji cha Maranje, kata ya Mtiniko Halmashauri ya Mji Nanyamba Mkoa wa Mtwara.
“Kongani hilo la viwanda linatarajiwa kuwa na viwanda 30 vya kubangua korosho, viwanda 6 vya kukamua mafuta ya ganda la korosho, viwanda 4 vya kusindika ufuta, na viwanda vya kutengeza bidhaa zitokanazo na mabibo ya korosho kama vile sharubati, mvinyo na pombe kali (ethanol) kwa ajili ya matumizi mbalimbali,” ameeleza Alfred na kubainisha kuwa,
“Kadhalika mpango uliopo ni kujenga maghala 100 za kuhifadhia mazao mbalimbali ikijumuisha mazao ya korosho na ufuta. Pia kutakuwa na huduma mbalimbali kama vile maduka makubwa, nyumba za kuishi wafanyakazi, viwanja vya michezo, migahawa, kituo cha polisi, jeshi la zimamoto, kituo cha kutoa huduma kwa wawekezaji, nk.Kwa sasa ujenzi wa miundombinu ya msingi kama vile maji, umeme, barabara na ujenzi wa ghala mbili za kuhifadhia korosho tani 10,000 kwa kila moja unaendelea,”.
Amesema mafanikio hayo yameletwa na juhudi zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye lengo la kuinua maisha ya wakulima na kuongeza mapato ya Serikali
Kuhusu maandalizi ya Mkutano huo, amesema Mkutano huo umendaliwa na Jukwaa la Korosho Afrika (ACA) kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania na Umoja wa Wabanguaji Wakubwa wa Korosho Tanzania (TACP) na utafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wabanguaji Wakubwa wa Korosho Tanzania (TACP) Bahati Mayona amesema Mkutano huo unategemewa kuhudhuriwa na washiriki wapatao 500 kutoka katika nchi zaidi ya 30 na hivyo kutoa fursa mbalimbali katika mnyororo wa zao la Korosho kwa maendeleo ya Tasnia ya korosho na Taifa kwa ujumla
Ametaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni pamoja na Ivory Coast, Cambodia, India, Vietnam, Brazil, Indonesia, Sri Lanka, Nigeria, Guinea Bissau, Burkina Faso, Mali, Benin, Ghana, Madagascar, Zambia, Msumbiji, Kenya, Mauritius, Visiwa vya Komoro na wenyeji Tanzania.