Kiongozi wa kisiasa wa kundi la waasi la M23 Corneille Nangaa ameapa kuwa wapiganaji wake hawatauachia mji wa Gomana kudokeza kuhusu azma ya kusonga mbele hadi mji mkuu Kinshasa. Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi.

Waasi wanaoungwa mkono na Rwanda ambao waliteka jiji kubwa la mashariki mwa Kongo walisema Alhamisi kuwa wanataka kupeleka mapgano yao hadi mji mkuu Kinshansa huku rais wa Kongo akihamasisha vijana kujiunga kwa wingi na jeshi kupambana na uasi, na waziri wake wa ulinzi akitupilia mbali wito wa mazungumzo. 

Katika ujumbe wa video Alhamisi, Waziri wa Ulinzi wa Kongo Guy Kabombo Muadiamvita alisema ametoa maagizo kwamba mipango ya mazungumzo yoyote na waasi “itupiliwe mbali mara moja.”  “Tutakaa hapa Kongo na kupigana. Ikiwa hatutaishi hapa, basi tutaishi wafu hapa,” alisema Muadiamvita, mshirika wa karibu wa rais wa Kongo.

Kiongozi wa kisiasa wa kundi la waasi la M23 ameahidi kuwa wapiganaji wake hawatakubali kuuachia mji wa Goma. “Tuko Goma na tutakaa hapa,” alisisitiza Corneille Nangaa katika mkutano na waandishi wa habari Alhamisi.

Hii ilikuwa ni taarifa ya kwanza ya umma kutoka M23 tangu wapiganaji wao kuchukuwa udhibiti wa Goma ambao unazunguka Ziwa Kivu, na ambao ni nyumbani kwa mamilioni ya watu mapema siku ya Jumatatu.

Nangaa ni kiongozi wa “Alliance Fleuve Congo,” kundi la kisiasa na kijeshi linalotaka kuipindua serikali ya Kinshasa. M23 ni mshirika muhimu zaidi katika kundi hili. Katika mkutano huo wa habari uliofanyika hotelini, Nangaa alivaa sare za kijeshi na alikaa katikati ya makamanda wa waasi.