Na Magrethy Katengu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema uzinduzi rasmi wa biashara kwa saa 24 utafanyika Februari 22, 2025 na utaanzia eneo la Ofisini za Mkuu wa Mkoa hadi Kariakoo kuwa na matukio tofauti tofauti.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Chalamila amesema ufanyaji biashara kwa saa 24 unalenga kuimarisha uchumi wa mkoa, kuongeza mapato ya serikali na kutoa fursa za ajira.

“Ufunguzi huo utaanzia ofisini za Mkuu wa Mkoa hadi Kariakoo ambapo ndipo watafanya ufunguzi rasmi.

Ameeleza kuwa maandalizi ya ufungaji wa kamera za CCTV na taa za barabarani yanaendelea ili kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unadumishwa.

“Tunahakikisha mkoa wetu wa Dar es Salaam unakuwa na mazingira bora ya kufanya biashara muda wote, na tayari tunashirikiana na viongozi wa halmashauri kuimarisha maeneo yanayofaa kwa biashara za masaa 24,” amesema Chalamila.

“Tutahakikisha tunapanga vizuri maeneo ya chakula pamoja na vinywaji ili kuweka mpangilio mzuri wa biashara hizo kwa kupangilia Usafi.

Aidha ameongeza kuwa mpango huo utaimarisha uchumi na kuwanufaisha wafanyabiashara na wakazi wa jiji hilo.

RC Chalamila amefafanua kuwa mji huo lazima ujengwe kwa kiwango cha kimataifa hivyo amebainisha kuwa tayari kamati imeshaundwa ya kukagua na kupitia majengo chakavu ambayo wanaoyamiliki wataombwa kuingia ubia na walio na uwezo kuyaendeleza ili kusaidia kutokuwepo kwa majengo yasiyo na hadhi ya kukaa katika ya mji.

Akizungumzia suala la ujenzi wa soko la Kariakoo Chalamila amesema zaidi ya bilioni 28 zimetolewa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo na kwamba ujenzi wake umefikia asilimia 97 pia amesema kwa sasa bodaboda na bajaji hazijazuiliwa kuingia katikati ya jiji kwani walizuiwa kwa siku chache kutokana na ugeni wa marais wa Afrika.

Kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Nishati uliofanyika Januari 27 hadi 28 Mwaka huu jijini Dar es Salama, RC Chalamila amewashukuru na kuwapongeza wananchi wa mkoa huo kwa ushirikiano mkubwa walioutoa ikiwemo kuimarisha amani, utulivu na usafi hivvyo ameelekeza wilaya zote kuendelea kusimamia suala la usafi ili Mkoa uendelee kuwa kivutio huku akisisitiza kuwa Serikali inakusudia kuanza kutumia usafiri wa treni na majini kuimarisha usafiri ndani ya jiji hilo.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Soko la Kariakoo Hawa Ghasia amesema kuanzia Januari 31 wanaanza kuweka majina ya wafanyabiaahara ambao walikuwepo kwenye soko la Kariakoo kabla halijaungua ili wasajiliwe na kwamba baada ya hapo watasajili wafanyabiashara wapya na waliokuwa wanadaiwa wanapaswa kulipa madeni yao.

” Januari 31 tunaanza zoezi la kuwarudisha waliokiwa wakifanya biashara lakini kwa masharti mtu anayejua anadaiwa huko nyuma alipe Kwanza deni Kwanza lote analodaiwa na TRA kwani hatutaruhusu kuingia kuwa wadaiwa sugu” amesema Hawa.