Na Mwandishi Wetu, Jamhurimedia, Iringa

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, amesema serikali inaridhishwa na kazi zinayofanywa na wakandarasi wanaojenga barabara za Mtili – Ifwagi (Km. 14) na Wenda – Mgama (Km. 19) ambazo zinagharimu bilioni 52.

Barabara hizo zinajengwa chini ya mradi wa RISE, unaofadhiliwa kupitia mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia, ukiwa na lengo la kurahisisha usafirishaji wa mazao ya misitu, mboga mboga, chai, na mazao mengine kutoka mashambani hadi sokoni kwa wakati.

 Moja ya daraja lililojengwa katika barabara ya Mtili-Ifwagi yenye urefu wa Km. 14 katika halmashauri ya Wilaya ya Mufindi

Akizungumza baada ya kuongoza kamati zinazohusika na usimamizi wa mradi huo katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi, Mhandisi Seff amesema miradi hiyo ipo katika hatua nzuri na akawataka wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha kazi kwa wakati uliopangwa ili kuboresha huduma kwa wananchi.

Aidha, amewataka wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya miradi kuwa walinzi wa kwanza wa barabara hizo ili kuzuia hujuma na wizi unaofanywa na watu wasio waaminifu, jambo ambalo limekuwa likisababisha hasara kwa serikali na kuhatarisha usalama wa miradi hiyo.

Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff akiongea na wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya mtili-Ifwagi ambayo inaelekea kwenye mashamba ya chai  ambapo  lengo la barabara hiyo ni kurahisha usafirishaji wa mazao ya misitu, mboga mboga, chai na mazao mengine .

Katika hatua nyingine, Mhandisi Seff ameagiza mkandarasi CHELESI GENERAL INTERPRISE anayetekeleza ujenzi wa barabara ya Ilula Image – Ilambo (Km. 40) kurejea kazini mara moja ili kukamilisha kazi hiyo na kuondoa vikwazo vya mawasiliano vilivyopo kwenye barabara hiyo.

Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hii ili kuhakikisha wananchi wananufaika kwa wakati na miundombinu inaboreshwa kwa ufanisi.

Ujenzi wa madaraja manne ya mawe yenye jumla ya urefu wa mita 70 yanayojengwa katika kijiji cha Isupilo Kata ya Lugemba ambapo yanaunganisha vijiji vya Isupilo na Ipimbo. Ujenzi huu ni utekelezaji wa uondoaji vikwanzo vya mawasiliano nchini unaofanya na TARURA kupitia mradi wa RISE.
Mafundi wakiendelea na upangaji wa mbao kwaajili ya ujenzi wa daraja la mawe katika kijiji cha Isupilo