Ndege ndogo iliyokuwa ikibeba wafanyakazi wa kisima cha mafuta kilichopo Jimbo la Unity, Sudan Kusini, imeanguka na kuua watu 20.
Waziri wa Habari wa Jimbo la Unity, Gatwech Bipal, amesema ndege hiyo ilianguka asubuhi jana Jumatano kwenye uwanja wa ndege wa Unity wakati ikiondoka kuelekea mji mkuu wa Juba.
Bipal alieleza kuwa abiria walikuwa wafanyakazi wa kampuni ya mafuta ya Greater Pioneer Operating Company (GPOC), inayojumuisha Shirika la Mafuta la Kitaifa la China pamoja na Shirika la Mafuta la Nile linalomilikiwa na serikali ya Sudan Kusini.
Miongoni mwa waliokufa ni raia wawili wa China na mmoja wa India, ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu chanzo cha ajali hiyo.