Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amemuapisha Michael Semindu kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Januari 25, 2025 kuwa mkuu wa wilaya hiyo.
Hafla ya uapisho huo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mjini huku viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa na wa dini wakihudhuria hafla hiyo.
Akizungumza baada ya tukio hilo RC Sendiga alimpongeza mkuu mpya wa Wilaya ya Mbulu na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza nguvu kazi ya watendaji katika Mkoa wa Manyara.
“Wakuu wa Wilaya Mimi kama kiongozi wenu, nina vipaumbele nilivyojiwekea ili kufikia malengo ya pamoja ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato ili serikali iweze kuwahudumia wananchi wake na kuleta maendeleo katika taifa, kipaumbele cha pili ni kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kuanzia ngazi ya mtaa mpaka katika halmashauri zao,”
“Cha tatu ni kusimamia ulinzi na usalama kwa kuweka mikakati ya kudhibiti uhalifu, cha nne ni kusimamia usafi wa mazingira ili kuweka mkoa katika hali ya usafi pamoja na usimamizi, ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” amesema Queen Sendiga.
Aidha anafafanua kuwa anatambua kuwa kila mmoja qmejiwekea vipaumbele vyake kama Mkuu wa Wilaya husika, hivyo kama Mkoa pia una vipaumbele vyake ambavyo kila mmoja anatakiwa kuvielewa na hatimaye kuweza kuvirekeleza.
“Naomba nendeni mkatimize wajibu wenu ipasavyo na mkatekeleze matarajio chanya ya Rais Samia Suluhu Hassan kwani amewaamini na ndio maana amewapa nafasi hizo, hivyo ukiaminiwa, nawe unatakiwa ujiaminishe ili kuweza kutimiza adhima hii kikamilifu.” amesema Sendiga.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semindu ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wenzake pamoja na kuyapokea maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kuyatekeleza majukumu yao yote kwa weledi mkubwa.