Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Baadhi ya wadau walipa kodi Mkoani Pwani, wametoa mapendekezo kwa Serikali kusaidia kupunguza utitiri wa kodi na ushuru ili kulinda mitaji yao na kujipatia faida kulingana na biashara zao.

Aidha, wameomba Serikali iweke mazingira bora ya kodi ili kila mmoja achangie pato la Taifa bila vikwazo.

Mwenyekiti wa TCCIA mkoani Pwani, Saidi Mfinanga, akitoa maoni kwenye kikao cha Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi na wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa kodi wilayani Kibaha, alieleza ,hakuna mfanyabiashara, mwekezaji, au mwananchi asiyetaka kulipa kodi au ushuru; changamoto ni kukosa mazingira rafiki ya ulipaji kodi.

Mfinanga aliomba, elimu ya mlipa kodi iendelee kutolewa kwa jamii, kuanzia mashuleni kuanzia elimu ya Msingi ili wanafunzi wawe na uelewa wa umuhimu wa kulipa kodi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani, Abdallah Ndauka, alipongeza hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume ya Maboresho ya Kodi, akisema kuwa itasaidia kuchakata mapendekezo na kisha kufanyiwa maboresho kwa manufaa ya walengwa.

Alitaja changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara ni kukosa uelewa kuhusu sheria na sera zinazohusiana na ulipaji kodi.

“Serikali iweke mfumo wa ulipaji kodi, ambapo mfanyabiashara akishalipa kodi, igawanye fedha hizo katika taasisi zake mbalimbali, kwani hali ya sasa inawachanganya wafanyabiashara kwa sababu TRA inakusanya kodi, Halmashauri inakusanya ushuru, na taasisi nyingine kama OSHA na NEMC zinatoza tozo na ushuru,” alisema Ndauka.

Alifafanua ,hali hiyo inakatisha tamaa na kuleta usumbufu kwa wafanyabiashara.

Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Balozi Maimuna Tarish, alieleza kuwa tume ina wajumbe tisa na inakusanya maoni ,kero na mapendekezo kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.

“Hatua hii inafanyika ili kufanya tathmini ya changamoto zilizopo na kisha kuzichakata kwa lengo la kufanya maboresho na kuondoa usumbufu.”

Aliongeza kuwa mara baada ya kumaliza kazi hiyo, tume itatoa ripoti na kuwasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili kufanyiwa maboresho, lengo kuu likiwa kuwainua wafanyabiashara wadogo kuwa wakubwa na kuhakikisha walipa kodi wanatoa kodi bila changamoto.

Naye Profesa Florens Luoga, ambaye ni Gavana mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania, alisema tume ya awali ilifanyia kazi changamoto za mlipa kodi miaka 35 iliyopita (1989), hivyo inafikia wakati mfumo uliopo lazima ufanyiwe maboresho.

Alisema, wananchi wasipolipa kodi itakuwa mzigo mkubwa kwa Serikali kwa sababu inatakiwa kufikia asilimia 20 ya pato la Taifa kwa mwaka ili Serikali iweze kujiendesha kwenye miradi yake.

Luoga alieleza kwamba kwa sasa tupo kwenye asilimia 11.9, na hii itawezekana endapo wigo wa walipa kodi utaendelea kuongezeka ili kufikia asilimia 20.

Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, alieleza kwamba mazingira ya kodi yanapaswa kuboreshwa ili kukabiliana na ushindani duniani.

Aliwataka wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kuendelea kutoa maoni na mapendekezo ili kufikia azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya mlipa kodi, kuanzia kwa wale wafanyabiashara wadogo.