Na Happy Lazaro, JamhuriMedia, Arusha
Wadau mbalimbali wa nishati kutoka ndani na nje ya nchi wamekutana mkoani Arusha kwa lengo la kujadili namna bora ya kuboresha sekta hiyo na kuweza kuweka mikakati ya pamoja katika kufikia malengo ya Dira ya mwaka 2030.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji TANESCO Mhandisi Costa Rubagumya amesema kuwa , mkutano huo unajadili mbinu na njia zitakazosaidia kufikia malengo ya Dira ya mwaka 2030, ambapo kwa Tanzania inatarajiwa kuwapatia wananchi milioni 8.3 kufikia mwaka 2030.
Mhandisi Rubagumya amesema ili kufikia mkakati huo uliowekwa, Shirika limejipanga kuhudumia wateja milioni moja na laki sita (1,600,000)kwa mwaka badala ya wateja laki tano (500,000)kama ilivyokuwa ikifanyika hapo awali.
“TANESCO limejipanga kuhakikisha linafikia lengo la kuwapatia wananchi wake umeme wa uhakika ili kuendana na Dira ya maendeleo ya upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa watu wapatao milioni 300 kati ya 600 kwa nchi za Afrika. .”amesema Mhandisi Rubagumya.
“Tunachokijadili hapa ni namna tutakavyoshirikiana katika uzalishaji wa umeme, usafirishaji na usambazaji na hata kufikia wale ambao walikuwa hawapati huduma ili waweze kupata kwa haraka na kuondokana na changamoto mbalimbali ” amefafanua Mhandisi Rubagumya.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ,Frank Mmbando amesema kwamba Serikali ya Mkoa wa Arusha imekuwa ikiweka mazingira wezeshi ya nishati ili kuhakikisha shughuli za uwekezaji zinafanikiwa.
“Nchi yetu imekuwa kinara na inaendelea kutajwa kwa wingi, hii ni baada ya kuanza biashara ya kuuza umeme katika nchi mbalimbali kama Kenya, Ethiopia, Uganda na Burundi” amefafanua Mmbando.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa shirika la umeme la nchini Kenya Joseph Siror amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki imeandaa mpango kwamba nishati zote zinazozalishwa, ziwekwe katika soko, ili wananchi waweze kununua na kutumia kwa bei nafuu.
“Bwawa la Nyerere Nchini Tanzania litakuwa mkombozi kwa kutoa umeme wa kutosha, na kusaidia Jumuiya hii hususan nchi zile ambazo hazijapata uwezo kama huu” amesema Siror.