*Ni kuhusu mabadiliko ya Katiba kuelekea Uchaguzi Mkuu

*Lissu asema yuko tayari kukutana na Rais Samia kuzungumzia hilo

*Wassira: Bunge linakaribia kuvunjwa, hakuna muda wa mabadiliko

*Mzee Kassori akosoa yaliyofanyika Mkutano Mkuu Maalumu CCM

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Vyama hasimu nchini vimeanza kutunishiana misuli huku kila upande ukitoa msimamo wake kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Msimamo mkali umeanza kuwekwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, akikazia hoja yake kwamba bila mabadiliko ya Katiba hawatashiriki uchaguzi huo wa Rais, wabunge na madiwani.

Akizungumza na Kituo cha Redio cha Bongo FM nyumbani kwake jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Lissu amesema kupitia Katiba, sheria na taasisi zilizopo hapa nchini kila kitu kimeharibika kuelekea uchaguzi huo.

“Tunataka mambo mapya, mfumo mpya wa uchaguzi, kwa muda uliobaki sijui kama itawezekana lakini hatuwezi kwenda katika uchaguzi kwa utaratibu huu. Kwani Mungu amesema lazima tufanye uchaguzi Oktoba au Novemba, hiyo ni amri ya Mungu?

“Kama unasogezwa ili tufanye marekebisho makubwa yanayohitajika mimi niko tayari kabisa, kwa sababu mfumo wa uchaguzi ukirekebishwa, ukawekwa sawa tutakwenda katika uchaguzi na wananchi watachagua viongozi wanaowataka lakini sasa hivi haiwezekani, kwa sababu mfumo wote umeharibika,” amesema.

Akijibu swali kuhusu msimamo wake kutaka uchaguzi usogezwe mbele kwa kuwa unavunja Katiba ya nchi, amesema kwa sasa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ina matatizo makubwa na haifai.

“Kwa sasa Katiba na sheria zetu hazifai, na inabidi tuzibadilishe. Tukisema tuifuate hiyo iliyopo sasa hivi maana yake itakuwa ni safari ya kwenda kuzimu,” amesema.

Pia amesema mabadiliko wanayoyataka hayatatokana na vikao watakavyofanya na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wassira, bali watakapofanya vikao na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mabadiliko hayo yatatokana na msimamo wa Rais Samia na serikali yake. Mchakato wa kutunga sheria ni wa kiserikali. Kabla sheria hamjaziona bungeni kwanza zinapita kwa Rais na zisipopita kwake hamtaziona bungeni.

“Mtu wa kumkaba si Wassira. Huyo atatupotezea muda na sisi hatuna muda wa kupoteza. Tutafanya kikao na Rais Samia kama itahitajika, kwa sababu mwenye uamuzi kuhusu masuala ya Katiba ni Rais, si Mwenyekiti wa CCM na hapa sizungumzii mambo ya siasa,” amesema.

Akijibu hoja hiyo wiki iliyopita jijini Dodoma, Wassira amesema msimamo wa Lissu kuhusu mabadiliko ya sheria kabla ya uchaguzi kufanyika hauna maana kwa sasa hivi.

“Hiyo kaulimbiu ya CHADEMA ya ‘No Reform, No Election’ haina maana yoyote, muda wa kufanya mabadiliko ya kisheria umekwisha kwa sasa, kwa sababu Uchaguzi Mkuu unakaribia kufanyika,” amesema. 

Badala ya kushikilia msimamo huo, amesema chama hicho kinapaswa kushiriki uchaguzi na kuhakikisha wanakubaliana na maridhiano yaliyopo. 

“Rais Samia na CCM wameonyesha utayari wa mazungumzo na Bunge linakaribia kuvunjwa, hivyo hakuna muda wa kufanya mabadiliko ya kisheria yanayohitaji muda mrefu,” amesema.

Amesisitiza uchaguzi wa mwaka huu unapaswa kuwa nafasi ya vyama vyote kushindana kwa hoja badala ya kutafuta visingizio na kuwataka viongozi wa CHADEMA kutumia nafasi za mazungumzo zilizopo badala ya kusimamia misimamo isiyotekelezeka kwa wakati huu.

“Ni muhimu kushiriki uchaguzi na kuwa sehemu ya demokrasia badala ya kupoteza muda na kauli ambazo hazina tija kwa wananchi,” amesema.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, amesema msimamo wa CHADEMA hauwahusu.

“Nataka niseme. Wana CCM hilo halituhusu. ‘Reforms’ zinafanywa na vyombo vya sheria ikiwamo Bunge. Sisi tumejiandaa na uchaguzi na hatuwezi kuelekezwa na mtu mmoja aseme ‘no reform, no election’. Mimi naamini wana ajenda ya siri na hawana fedha ya uchaguzi na hawajajipanga na uchaguzi.

“Wanatafuta visingizio. Wajipange, ‘reforms’ zipo, safari hii tutakuwa na tume huru ya uchaguzi, hakuna watu kupita bila kupingwa, na hayo ni mabadiliko makubwa, hayakuwapo na hizo reforms haziwezi zikaelekezwa kama matamko,” amesema akiwa katika ziara ya chama hicho iliyoanza Zanzibar juzi.

Pia amesema kuna vyama 18 vilivyosajiliwa hapa nchini na haiwezekani chama kimoja kikawa na uwezo wa kuelekeza.

“Rais Samia ni muumini wa 4R na kama kuna jambo linaongelewa ni la wadau wengi na si mtu mmoja,” amesema.

Mwenendo wa siasa kubadilika

Katika hatua nyingine, Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Richard Mbunda, ameliambia JAMHURI kwamba misimamo ya Lissu baada ya kushinda uenyekiti itabadilisha mwenendo wa siasa za hapa nchini, ikiwamo hoja yake ya kutaka mabadiliko ya sheria kuelekea uchaguzi.

“Mambo yanabadilika, watu walikuwa hawana imani kwamba Lissu anaweza akashinda nafasi ya uenyekiti kutokana na nafasi ya mwenyekiti aliyekuwapo.

“Tathmini yangu ya haraka Lissu ni rahisi kusambaza moto wa mabadiliko nje ya chama na utaleta athari kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Hili nina uhakika nalo,” amesema.

Pia amesema uwezo wa Lissu wa kuendesha siasa za harakati ni kigezo kitakachochochea mabadiliko ya siasa hapa nchini na zitakuwa za hekaheka japo anautilia shaka msimamo wake wa kutaka mabadiliko ya sheria kabla ya uchaguzi.

“Msimamo wake wa kutaka mabadiliko ya sheria ya uchaguzi yafanyike haraka ninautilia shaka kwa sababu muda uliosalia huenda hilo lisifanyike, badala yake likaibua mvutano dhidi ya chama tawala,” amesema.

Naye Katibu Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, amesema kwamba kwa kipindi kirefu Watanzania wanalalamikia ukosefu wa demokrasia hasa katika mifumo ya uchaguzi.

“Ni lazima tufike mahali mifumo yetu ya uchaguzi iboreshwe, watu wanaoisimamia wasiwe ndio hao hao wenye uamuzi wa kuteua watu wa kugombea na kuisimamia,” amesema.

Pia ameshauri wasimamizi wa uchaguzi nchini kama vile Mwenyekiti wa INEC awe anachaguliwa na Bunge badala ya kuchaguliwa na Rais, akiamini hatua hiyo inaweza kutengeneza mazingira mazuri ya uchaguzi huru na haki.

Kuhusu msimamo wa Lissu kuwa bila mabadiliko ya Katiba hakuna uchaguzi, ameshauri badala ya kufanya maboresho makubwa kabla ya uchaguzi yafanyike madogo hasa yanayohusu sheria za uchaguzi, akiamini kwa sasa mchakato huo hauwezi kufanyika.

“Labda kama nchi tukubaliane tusogeze uchaguzi mbele ili tufanye mabadiliko ya katiba, hili linawezekana kama tukitaka,” amesema.

Pia amesema vyama vya upinzani, CCM pamoja na dola vinatakiwa kukubaliana na kutazama maeneo yenye kasoro katika Katiba ili yaboreshwe.

“Shida kubwa iliyopo si Katiba wala sheria, shida kubwa ni namna ya kuisimamia, hakuna sheria inaruhusu watu kuenguliwa bila sababu za msingi, sidhani kama kuna sheria imeelekeza hivyo, lakini unaweza kuona watu wanashindwa kusimamia hata sheria zilizopo,” amesema.

Mzee Kassori aonya

Kwa upande mwingine, mmoja kati ya wazee wa CCM, Samweli Kassori, ameukosoa utaratibu uliotumika kumpitisha Dk. Samia kuwa mgombea wa urais kupitia CCM, akisema kulikuwapo kasoro za wazi.

Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliofanyika Januari 18 na 19 jijini Dodoma pia ulimpitisha Dk. Hussein Ali Mwinyi kuwa mgombea wa CCM Zanzibar.

“Ni makosa. CCM wamekiuka utaratibu. Awali nilimlaumu Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, nikisema alipaswa kuwashauri viongozi wa CCM kabla ya kuwapitisha Rais Samia na Dk. Mwinyi.

“Lakini kwa hakika aliyekosea ni Kikwete (Rais wa Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete). Kikwete alipaswa kushauri mkutano uahirishwe kwa dakka kadhaa, wakafanye majadiliano ndipo warejee na kuwaomba wajumbe ajenda zilizokuwapo ziendelee,” amesema.

Kassori, aliyekuwa Katibu Myeka wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, anasema si sahihi kwa Mkutano Mkuu Maalumu kupitisha wagombea hata kabla ya kuchukua fomu.

Amehoji ni nani aliyewatuma wajumbe 2,000 tu wa Mkutano Mkuu Maalumu kupitisha hoja nzito kiasi kile?

“CCM ina wanachama zaidi ya milioni 5, sasa hawa kweli wamewatuma? Mimi sina shaka kwamba Rais Samia na Dk. Mwinyi watapita, lakini kwa nini kuharibu utaratibu?” anahoji Kassori.

Anashangaa ni kwa nini wajumbe wasiendelee kujadili ajenda ya Ilani ya Uchaguzi iliyokuwa mezani badala yake wakaitupa kapuni, ilhali ilikuwa na masuala nyeti na muhimu kwa Watanzania!

“Binafsi niliondoka Dodoma kwa masikitiko makubwa sana kwa wajumbe. Hawa, kwa sababu wanazozijua wao wamewanyima Watanzania haki yao ya msingi ya kusikiliza majadiliano ya taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.

“Ilani iliyowashawishi Watanzania kuipigia kura CCM kipindi cha 2020 hadi 2025. Watendaji walikuwapo, lakini mjadala haukufanyika. Walimu wa Zanzibar wanaishi kwenye nyumba nzuri, hawaishi mitaani. Kwa nini Tanzania Bara tusiige? Na hilo lingefanyika kama Mkutano Mkuu Maalumu ungejadili utekelezaji wa Ilani,” amesema.