Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Mkuu wa Shule ya Sekondari Ruvuma mwalimu Atemius Komba ameishukuru Serikali kwa kuwapatia pesa sh. milioni 278.4 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 11 na matundu ya 8 ya choo cha wasichana.

Hayo ameyasema jana wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahamed Abbas Ahamed alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua mradi huo.

Moja ya madarasa 11 katika shule ya sekondari Ruvuma yaliyojengwa na serikali kuu ambayo yamegharimu kiasi cha sh milioni 278.4

Alisema kuwa Juni 24 / 2024 walipokea pesa kutoka Serikali Kuu kiasi cha sh. Milioni 278.4 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 11 yaliyogharimu kiasi cha sh. Milioni 264 na matundu 8 ya choo kwa gharama ya sh. Milioni 14.4.

Alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Septemba 1/2024 ambapo kazi ziligawanywa katika makundi matano ili kuharakisha utekelezaji na kuwapatia mafundi ambao hadi hadi kufikia Januari 26 /2025 utekelezaji wa mradi ulifikia asilimia 95 hata hivyo kazi zingine za ukamilishaji zinaendelea.

Alieleza zaidi kuwa hadi kufikia Januari 27 / 2025 kiasi cha fedha sh. Milioni 270.7 kati ya sh. Milioni 278.4 zilizotolewa zimetumika na kubakiwa na salio la sh. Milioni 7.6 ambazo zitakidhi kukamilisha kazi ndogo ndogo zilizobaki.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahamed Abbas Ahamed akikaguwa Ujenzi wa matundu ya vyoo 8 kwaajiri ya wasichana katika shule ya sekondari Ruvuma

Aidha ameishukuru Serikali chini ya Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu ili kuinua kiwango cha elimu na kuboresha ustawi wa wananchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahamed Abbas Ahamed amezipongeza kamati za manunuzi, ujenzi na isimamizi kwa kazi nzuri iliyofanyika kwa asilimia walizozitaja na kwamba matumizi ya fedha yamefanyika vizuri na fedha zilizobaki kiasi cha sh. Milioni 7.6 itaenda kumalizia kazi ndogo ndogo zilizobaki.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahamed Abbas Ahamed akiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari Ruvuma