*Ahofu mgogoro wa Simba utaathiri soka nchini
Mwanachama wa siku nyingi wa Wekundu wa Msimbazi, Simba Sports Club ya Dar es Salaam, Dk. Mohamed Wande, ametaja mbinu pekee ya kuinusuru klabu hiyo isididimie kisoka kuwa ni mshikamano wa wanachama na wachezaji.
Pia ameeleza wasiwasi wake kwamba mgogoro unaoendelea ndani ya Simba, unaweza kuathiri tasnia ya soka nchini.
Dk. Wande ameeleza changamoto hizo katika mahojiano maalumu na JAMHURI jijini Dar es Salaam, hivi karibuni.
“Hali si shwari ndani ya Simba, kwa sababu hiyo kuna haja ya kuwaunganisha wanachama na wachezaji wa klabu hii, ili isiendelee kudidimia,” amesema Dk. Wande na kuendelea:
“Ninasisitiza hilo kwa sababu mgogoro ukiachwa uendelee ndani ya Simba, hautaathiri Simba pekee bali hata tasnia ya soka nchini kutokana ukubwa wa klabu hii.”
Huku akisisitiza kuwa hana ugomvi binafsi na viongozi wa Simba, Dk. Wande amesema kinachowaponza ni kutoisimamia vizuri na kujiamulia baadhi ya mambo yanayoihusu klabu hiyo.
“Siku zote nimekuwa nikisema, na ninaendelea kusema kwamba uongozi wa Simba hauko makini katika kuongoza na kusimamia klabu,” amesema na kuongeza:
“Ni kweli kwamba timu ya Simba ilianza kufanya vibaya kabla ya mgogoro uliopo, lakini ni wazi kuwa mgogoro huu umeifanya Simba kufanya vibaya zaidi.”
Kwa mujibu wa Dk. Wande, idadi kubwa ya wanachama wa Simba hawakuridhishwa na uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wa kuishauri klabu hiyo ifanye mkutano mkuu Julai, mwaka huu.
“Wanachama wengi tumekosa matumaini kwa TFF, sasa hivi tunasubiri uamuzi wa Msajili wa Klabu kuhusu mgogoro uliopo, ndiye tegemeo letu,” amesema.
Ameongeza kwamba kutokomezwa kwa matatizo ndani ya Simba, kutaiwezesha klabu hiyo kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.
Pamoja na malalamiko mengine, wanachama wa Simba wamekuwa wakimtuhumu Mwenyekiti wa klabu, Ismail Aden Rage, kuwa ameshindwa kusimamia vizuri timu yao kiasi cha kuifanya ionekane kudorora kisoka.
Machi 17, mwaka huu, baadhi ya wanachama wa klabu hiyo waliitisha mkutano na kumng’oa mwenyekiti wao huyo, lakini TFF ilijitokeza na kutangaza kutotambua mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Starlight jijini Dar es Salaam.