Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Usimamizi la Mazingira la Taifa (NEMC) imeupongeza uongozi wa kampuni ya Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kulinda ikolojia ya Mto Sigi na kuhifadhi mazingira katika mikoa yote bomba linakopita.

Mto Sigi una sifa za kipekee duniani na kwa hiyo EACOP imejenga taneli maalum ambamo bomba linapita chini ya mto na kwa hiyo kuhakikisha hayatokei madhara yoyote katika mfumo wa ikolojia ya mto huo.

Akizungumza hapa wakati wa ziara ya wajumbe wa bodi hiyo hivi karibuni katika Rasi ya Chongoleani, Mwenyekiti wa bodi hiyo , Prof. Esnat Chaggu, alisema kwamba bodi inapongeza uamuzi wa kupitisha bomba chini ya Mto Sigi kwa kuwa hatua hiyo inalinda mazingira na mfumo wa ikolojia ya mto huo. EACOP inajenga Chongoleani temino ya kusafirisha mafuta kwenda kwenye masoko ya kimataifa.

Mto Sigi una umaarufu wa kimataifa kwa sababu chanzo chake ni Milima ya Usambara Mashariki na misitu yake. Eneo hilo, linalojulikama kama Hifadhi ya Asili ya Amani, lina sifa za kuwa na viumbe na mimea ambavyo havipatikani kwingineko duniani. Mto Sigi hutiririsha maji kutoka Milima ya Usambara Mashariki hadi Bahari ya Hindi.

“Kupitisha bomba chini ya Mto Sigi, ni mafanikio makubwa katika ujenzi wa mradi na ni kielelezo cha usimamizi wa mazingira kwa sababu hatua hiyo ni ushahidi wa kulinda maisha ya viumbe vya majini na ubora wa maji,” alisema Prof. Chaggu.

Alisema kuwa wajume wamefurahishwa na utaalamu unaotumika katika kuhifadhi mazingira ya mto huo wenye thamini kubwa kimazingira duniani.

Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali (mstaafu) Fred Mwesigye (katikati) akioneshwa maendeleo ya mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) na Mhandisi wa mradi huo kutoka EACOP, Musa Msafiri (kushoto) wakati wa ziara ya maofisa wa Ubalozi wa Uganda nchini Tanzania mara baada ya kuwasili kwenye eneo la mradi huo katika kijiji cha Chongoleani mkoani Tanga hivi karibuni

“Wakati wa ziara yetu, tulifurahi kuona jinsi mradi wa EACOP unavyozingatia kikamilifu sheria za mazingira za kitaifa na kimataifa, Mradi unahakikisha kuwa unafanya kazi katika njia bora za uhifadhi wa mazingira,” aliongeza.

Mratibu wa Masuala ya Mazingira wa EACOP, Bw Joflin Bejumula, aliuleza ujumbe kuwa mradi unazingatia sheria zote muhimu za mazingira ili kuepuka madhara ya aina yote kwa jamii zinazouzunguka mradi na mazingira kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa mradi unajitolea kulinda mazingira asilia wakati wote wa utekelezaji wake.

Bomba la EACOP lina jumla ya kilomita 1,443 kutoka Wilaya ya Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, ambapo kati ya kilomita hizo, kilomita 1,147 zipo nchini Tanzania.

Mradi huu umefanikiwa kupunguza madhara ya kimazingira, kwa sababu utekelezaji wake umetanguliwa tathmini mbalimbali.

Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali (mstaafu) Fred Mwesigye (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na maofisa wengine wa ubalozi huo hapa nchini na wafanyakazi wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) wakati wa ziara ya siku moja kujionea maendeleo ya mradi huo katika kijiji cha Chongoleani mkoani Tanga hivi karibuni.

Imeelezwa pia kuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya mradi huu inatokana na ushirikiano wa karibu kati ya mradi na jamii za maeneo ya mradi, hasa jamii zinazoguswa moja kwa moja na njia ya bomba. Ushirikiano huo umewezesha kuongezeka kwa ufahamu wa jamii juu ya athari zinazoweza kutokea kimazingira na kuweka mikakati bora ya kupunguza athari hizo.

Bw Bejumula alieleza pia kuwa mradi unaendelea kutekeleza hatua mbalimbali za uhifadhi wa mazingira, ikiwemo uhifadhi wa maisha ya baharini, ulinzi wa wanyamapori, na juhudi za kupunguza kelele, mitetemo, na hatari ya kuvuja kwa mafuta.

Washirika wa mradi wa EACOP ni pamoja na TotalEnergies yenye asilimia 62%, mashirika ya kusimamia nishati ya mafuta nchini Tanzania (TPDC) na Uganda ( UNOC) yenye asilimia 15 kila moja na Shirika la Mafuta la China (CNOOC) lenye asilimia 8 ya hisa.