Na Mwandishi Wetu- Jeshi la Polisi, Arusha
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha leo Januari 24, 2025 limekabidhiwa pikipiki 20 ambazo zimetolewa na Taasisi ya Leopard Tours kwa ajili ya kuimarisha usalama mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda wakati akikabidhi pikipiki hizo katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Mkuu wa Mkoa ameishukuru taasisi hiyo kwa uthubutu wake wa kurudisha kwa jamii kwa kulipatia Jeshi la Polisi vitendea kazi ambavyo vitasaidia kutekeleza majukumu yao vyema ya kuimarisha usalama.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoani humo kwa namna ambavyo walihakikisha sikukuu za mwisho wa mwaka zinafanyika katika hali ya amani na utulivu bila kuwepo kwa matukio ya uvunjifu wa amani, na kuwataka kuongeza kasi ya kuimarisha usalama ili Mkoa huo uendelee kuwa shwari.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Leopard Tours Bw. Zuher Lazal amesema kuwa taasisi hiyo imetoa pikipiki hizo kutokana na juhudi zilizowekwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya utalii hali inayopelekea kurudisha kwa jamii kwa kutoa misaada mbalimbali ikiwemo pikipiki hizo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo pamoja na kumshukuru Mkuu wa Mkoa kwa namna ambavyo amekuwa akiwapatia vitendea kazi, amesema watahakikisha Mkoa wa Arusha unaendelea kuwa shwari wakati wote hasa kwa kuzingatia ni kitovu cha utalii hapa nchini.