Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa mvua za msimu wa Masika Machi hadi Mei 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 23, 2025 jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema mvua za wastani hadi juu ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki pamoja na Mashariki mwa mikoa ya Mara na Simiyu.
Dkt. Chang’a ameongeza kuwa mvua za wastani hadi chini ya wastani zinarajiwa katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini, Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na Ukanda wa Ziwa Victoria.
“Mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki pamoja na Mashariki mwa Mikoa ya Mara na Simiyu,” amesema Dkt. Chang’a na kuongeza,
“Aidha, mvua za wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini, Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na Ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na magharibi mwa mikoa ya Simiyu na Mara) katika kipindi cha Msimu wa Masika, 2025,”.
Ameongeza kuwa, ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Aprili 2025, ambapo ametoa angalizo la matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vipindi vya mvua kubwa kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi Chini ya wastani.
Kuhusu athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a amesema Mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo zinaweza kupelekea upungufu wa upatikanaji wa maji kwa matumizi ya majumbani, kilimo na ufugaji.