Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema mwaka uliopita 2024 umevunja rekodi kwa ongezeko la joto duniani likiongezeka kwa nyuzi joto 1.55.
Akizungumza kwenye warsha ya wanahabari juu ya Utabiri wa Mvua za Msimu wa Masika leo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a amesema ongezeko hilo ni la dunia huku kwa Tanzania joto likiongezeka kwa nyuzi joto 0.7 likiwa ni ongezeko la juu zaidi kurekodiwa.
“Hii yote inatokana ma mabadiliko ya hali ya hewa ambayo dunia inakutana nayo, kwa rekodi kuanzia mwaka 2023, inaonyesha joto litaendelea kuongezeka zaidi duniani,” amesema Dk.Chang’a.
Amesema juhudi zaidi zinatakiwa katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani kote ili kupunguza ongezeko hilo la joto.
Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi huyo ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya hali ya hewa katika miundombinu na rasilimali watu.
“Katika kupindi cha mwaka jana, serikali imewezesha ukamilishaji wa ujenzi wa rada mbili katika mikoa ya Kigoma na Mbeya, hii inafanya kwa Afrika Mashariki kuwa nchi kinara kwenye miundombinu ya hali ya hewa,” amesema Dk Chang’a.
Kwa upande wa ujuzi, amesema Mamlaka hiyo ina wafanyakazi 560 na kati ya hao wafanyakazi 80 wapo.mafunzo ndani na nje ya nchi sawa na asilimia 15 ya wafanyakazi wote.
“Kwa uwekezaji huu unatupa fursa wa kuendelea kuwa kitovu cha ubora katika masuala ya hali ya hewa Afrika, sababu za kuwa hivyo tunayo na uwezo pia tunao kutokana na uwekezaji unaofanywa na serikali, ili nimelisema mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizindua mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani wa ‘Systematic Observation Fanancing Facility’ kule Dodoma, jana”, amesema Dk Chang’a.
Wakati huo huo, TMA imetoa wataalamu wawili wa Hali ya Hewa kwenda nchini Burundi kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalam wa nchi hiyo.
Amesema wenzao wa Burundi wameoomba kupatiwa wataalam hao ili kuwajengea uwezo wafanyakazi wao Mamlaka ya Hali ya hewa.
“Tunatarajia wataalam wetu wawili kesho (leo) wataelekea Burundi baada ya maombi ya wenzetu, hii inaonyesha ni namna gani tumekuwa na wataalam wengu kutokana na uwekezaji wa Serikali katika kuwajengea uwezo wataalam wa TMA,” amesema Chang’a.