Na Kambi Mbwana, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho ndicho chama kikuu cha upinzani nchini, leo kinafanya uchaguzi wa viongozi wao.
Katika uchaguzi huu, nafasi ya Mwenyekiti na Makamu wake zimekuwa na joto kali.
Wanaowania nafasi hizo wamegawanyika katika makundi mawili yenye uhasimu mkubwa.
Aliyeshika nafasi ya uenyekiti kwa zaidi ya miaka 20, Freeman Mbowe, anaomba tena kuchaguliwa; huku Makamu wake, Tundu Lissu, akijitosa kuitaka nafasi hiyo hiyo!
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti inawaniwa na wanachama waandamizi; John Heche na Ezekia Wenje.
Ili kuongeza joto, wawili hawa wamejigawa katika kambi mbili, Heche akijitangaza kumuunga mkono Lissu; Wenje akiwa upande wa Mbowe.
Ni wanachama ndio watakaoamua nani anastahili na yupi asiyestahili.
Katika kuwashawishi wajumbe, mambo mengi yanasemwa. Yapo yenye ukweli na mengine yanasemwa tu ilimradi wapate uungwaji mkono ndani ya CHADEMA.
Kwa nini nasema hivi? Tangu kuanza kwa kampeni za CHADEMA, jina ‘Abdul’ limetamkwa mara nyingi na baadhi ya wagombea; akihusishwa na hila ovu.
Jina lake kamili ni Abdul Hafidh Ameir, ni mtoto wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Si mara moja au mbili, Lissu amemtaja Abdul pasi na ushahidi wa kutosha, akisema alitaka kumhonga fedha. Lissu ahongwe ili iweje?
Kana kwamba haitoshi, anamtaja Wenje kuwa ndiye aliyemuunganisha na Abdul. Hoja hii haina ukweli. Anasema kustawisha kambi yake ya uchaguzi.
Ndiyo, anayedaiwa kumuunganisha Lissu na Abdul ni Wenje, ambaye anamuunga mkono Mbowe; si Lissu.
Ingekuwaje kama Heche ndiye Wenje? Lissu angetoka hadharani kusema alimuunganisha na mtoto wa Rais ili ahongwe? Inakumbukwa kuwa ni kambi ya Lissu iliyosambaza propaganda za madai kuwa mwenyekiti wao ‘amelamba asali’.
Hata huu uchaguzi unaofanyika leo, wanasema umedhaminiwa na Serikali ya Dk. Samia. Hoja hii nayo ni dhaifu. Imeanzishwa kwa makusudi, kwa lengo la kumchafua Abdul na serikali inayoongozwa na Rais ambaye yeye ni mama yake mzazi.
Lissu ni mwanasiasa. Wanasiasa wengi wana kawaida ya kuzungumza chochote watakachohisi kitawapa umaarufu hata kama ni kwa kuumiza upande mwingine.
Ndivyo wanasiasa walivvyo duniani kote. Wenje angekuwa anamuunga mkono Lissu, hoja ya kuhongana isingekuwapo kwa sababu ingeharibu ‘mtandao’ wake.
Kwani hoja ya Edward Ngoyai Lowassa kwamba ni fisadi iliishia wapi? Ni kina Lissu na wenzake waliokuwa wanamchafua alipokuwa waziri mkuu; ghafla wakabadilika alipohamia CHADEMA na kuanza kumsafisha wakijua ujio wake unatija kwao.
Kwenye uchaguzi wa CHADEMA leo, kama wajumbe wanamhitaji Lissu awe mwenyekiti wao, basi wasiangalie hoja ya Abdul kwani ni ya uongo.
Imeanzishwa kwa makusudi kwa kuamini kumtaja Abdul, ni kumgusa pia Rais Samia, kiongozi wa nchi mwenye heshima na ushawishi mkubwa ndani na nje ya nchi.
Unapotaja viongozi wa nchi wenye heshima, jina la Rais Samia litaongoza kati ya watakaotajwa. Heshima yake inatokana na uchapa kazi wake.
Kwa miaka minne tu, amejikusanyia shahada tano za udaktari wa heshima kutoka vyuo vikuu mbalimbali duniani.
Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea (KAU) kimemtunuku Rais Samia Shahada ya Udaktari wa Heshima (PhD) Juni 3, 2024 jijini Seoul, Korea.
Hii ilitokana na mchango wake katika kuboresha sekta ya anga nchini tangu aingie madarakani Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Dk. John Magufuli, aliyefariki dunia Machi 17, 2021.
Kama hiyo haitoshi, Dk. Samia pia ametunukiwa shahada na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Jahawal Nehru cha India na Chuo Kikuu cha Antaria Uturuki.
Ikiwa vyuo vyote hivi vimeona heshima ya Rais, haiwezi kubagazwa na mtu mmoja anayetafuta masilahi ya kisiasa.
Pengine ni kweli watu hawa wamekutana katika majadiliano kama alivyosema Lissu, lakini kwamba amekwenda na begi la pesa ili amhonge! Huo ni uongo.
Kwa wanaofuatilia siasa za Tanzania, hii si mara moja mtoto wa Rais kupakwa matope na wanasiasa bila ukweli wowote.
Rejea kipindi cha uongozi wa Dk. Jakaya Kikwete, Rais wa Nne wa Tanzania. Mtoto wake, Ridhiwan, alikutana na joto kama hili la Abdul, akitajwa kuwa na hisa katika kila mradi mkubwa nchini.
Miradi iliyoendelezwa kwenye Hifadhi za Taifa kama hoteli, vituo vya mafuta, mabasi, supamaketi zote za Dar es Salaam, zilikuwa mali ya Ridhiwan.
Bahati mbaya waliokuwa wanamsema Ridhiwan kwa sababu ya urais wa baba yake, ndio hao hao leo wanamsema Abdul kwa nia ile ile.
Miaka ya 2010 hadi 2015 nilikwenda katika ofisi ya uwakili ya Ridhiwan pale Maktaba ya Taifa ili tu nimwone mtu aliyetajwa kama tajiri namba moja mjini. Kwamba kila kitu kizuri jijini Dar es Salaam kilikuwa chake.
Leo sina uhakika kama utajiri wake unaendelea! Badala yake watu wamehamia kwa Abdul. Ninaamini kinachosemwa leo ni fimbo ya kumchapia Dk. Samia kutokana na utendaji kazi wake.
Siasa za leo ni ngumu kwa wapinzani. Dk. Samia amekuwa muwazi, kiunganishi cha Watanzania kupitia falsafa ya ‘R Nne’ iliyowanufaisha wanasiasa wa Tanzania, akiwamo Lissu.
Ni kipindi cha Rais Samia wote waliokimbilia nje ya nchi wamerudi kulijenga taifa. Harakati anazofanya Lissu akishirikiana na kina Godbless Lema, Heche na wengeneo zinatokana na jitihada za Dk. Samia.
Badala ya kutafuta hoja nyepesi kumuadhibu, wanapaswa kumpongeza kwa moyo na mchango wake wa kuweka sawa mazingira ya kisiasa nchini.
Watanzania na wafuasi wa siasa za vyama vingi hususan CHADEMA wanaofanya uchaguzi leo, waelewe yote yanayosemwa juu ya Abdul ni fimbo ya kumchapia mama yake.
Endapo urais wa Dk. Samia utakoma, hoja hizi zitakufa kama zilivyokufa zile dhidi ya Ridhiwan. Ni ajabu! Lissu na kundi lake walipaswa wawaonyeshe wafuasi wao wanataka kuifanyia nini CHADEMA!
Lakini kutafuta hoja kutoka nje ya chama chao ili waonekane wanajua kuzungumza, si sahihi. Ni uchochezi. Ni kuchafuana. Wapiga kura wa CHADEMA wanapaswa kuzipuuza na kujadili hoja zinazoweza kulivusha taifa, si kulisambaratisha.
Tuangalie dhamira ya dhati ya Dk. Samia juu ya nchi yetu. Ustahimilivu wake unahitaji kuungwa mkono. Ndiyo maana pamoja na hoja chafu zinazosemwa na baadhi ya wagombea wa nafasi za uongozi wa juu wa CHADEMA, lakini zinapuuzwa.
Huu ndio ukweli. Hata Lema alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Januari 17, 2025, alikiri ni kwa namna gani amenufaishwa na uwepo wa Rais Samia.
Si Lema tu, Watanzania wengi tunafurahishwa na uwepo wa Rais Samia. Hata kama wachache watashindwa kuona mazuri, tulio wengi tutasimama hadharani kulizungumzia hili bila woga.
0712053949