*Haijapata kutokea: Yeye, wenzake wapitishwa bila kujaza fomu

*Dk. Mwinyi akabidhiwa bendera ya CCM urais Zanzibar

*Dk. Nchimbi apitishwa kuwania u-Makamu wa Rais kumrithi Dk. Mpango

*Wasira ‘Tyson’ akabidhiwa mikoba CCM Tanzania Bara

Na Waandishi Wetu, Dodoma, Dar

Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma, umekuwa ni wa aina yake ukiandika historia mpya nchini.

Wagombea wa nafasi za juu kabisa za uongozi wa nchi wamepitishwa kwenye mkutano mkuu kwa azimio bila kujaza fomu kuwania nafasi hizo, jambo ambalo halijawahi kutokea.

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alitoa hoja ya kumtaka Rais Samia Suluhu Hassan atoke kwenye kikao ili Mkutano Mkuu Maalum umjadili na umtendee jambo.

Rais Samia alijibu hoja hiyo akisema kuwa yeye ndiye Mwenyekiti na anapaswa kusimamia mkutano kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Baada ya kauli hiyo ya Rais Samia, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma Adam Kimbisa, yeye alipasua yai. Akasema: “Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM ufanye uamuzi, kwamba Rais Samia ndiye awe mgombea pekee wa urais kwa tiketi ya CCM.”

Ukumbi ukalipuka kwa shangwe. Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete alibaini kuwa Rais Samia amepigwa na butwaa kutokana na hoja hii ambayo ilishangiliwa kwa nguvu kubwa.

Kutokana ukongwe na uzoefu wake, Kikwete akapendekeza kuwa sasa badala ya kila mtu kusema tu, basi lipitishwe azimio la kwamba Dk. Samia ndiye mgombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Katika mazingira hayo, Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais Samia, akaagiza Sekretarieti ikaandae Azimio, lisomwe, kisha lipitishwe na wajumbe.

Awali, mkutano huo uliitishwa maalumu kwa ajili ya kumpitisha Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Komredi Abdulhaman Kinana aliyejiuzulu.

Lakini ghafla, upepo ukabadilika baada ya wajumbe kupitisha azimio kumtaka Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu; huku Makamu Mwenyekiti CCM Tanzania Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akipitishwa kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wakampitisha Samia kwa azimio la kauli moja ya asilimia 100 ya kura zote 1,924 zilizopigwa. Hakuna kura iliyoharibika.

Mambo hayakuishia hapo. Wakati Dk. Samia akiwashukuru wajumbe huku akisema wamemsababishia mshangao wa mwaka, kana kwamba ni kulipa kisasi; naye akaja na jambo jingine lililowaacha wengi midomo wazi kwa mshangao, kama si mshtuko.

Rais alisema kwa utaratibu wa CCM akipatikana mgombea urais, anapaaswa kumpata mgombea mwenza, hivyo akaomba kamati kuu watoke wakatete kidogo kupata jina la mgombea mwenza.

Ukumbini watu wakabaki na mshangao, maana walijua baada ya kumpata mgombea urais, mambo ya mgombea mwenza yangekuwa katika mkutano mkuu wa Julai.

“Kwa hiyo sasa naomba Kamati Kuu tutoke tukatete ili tuje na jina la Mgombea Mwenza,” alisema Dk. Samia, katika mwendelezo wa matukio ya aina yake kuwahi kufanywa kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM.

Rais Samia alisema: “Dk. Mpango aliniomba, akisema kwa umri wake; miaka 68 sasa, angeomba kupumzika. Sikumjibu. Akaamua kuniletea barua. Hata nayo sikumjibu. Lakini alipojieleza mbele ya wajumbe wa kamati kuu, kwa pamoja tukamkubalia.”

Huku ukumbi ukiwa kimya kwa kiwango ambacho hata ungedondosha sindani ingesikika, Rais alivuta pumzi kidogo, baadaye akasema:

“Tumemteua kijana wetu (akasita) Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.” Ukumbi ukalipuka kwa shangwe

Rais Samia alisema kwa kumteua Dk. Nchimbi kuwa mgombea mwenza, kuna tatizo jingine litajitokeza la ukatibu mkuu wa CCM, hata hivyo akafafanua kwamba kwa sasa viongozi wote wawili; Dk. Mpango na Balozi Dk. Nchimbi wataendelea na majukumu yao ya sasa hadi baadaye.

Wadau wanasemaje?

Akizungumza na JAMHURI kuhusu kupitishwa kwa Dk. Samia kuwa mgombea wa CCM kwenye uchaguzi ujao, Mbunge wa zamani wa Mpanda Kati, Said Arfi, amesema ni uamuzi wa busara.

“Mkutano Mkuu uliofikia uamuzi huu ni mkutano halali kikatiba. Ndiyo wenye mamlaka ya kuteua mgombea. Nadhani wajumbe wamefanya hivi, pamoja na mambo mengine, kukipunguzia chama gharama kwa kuwa ni wao hao hao ndio wangerudi tena Julai kufanya uteuzi,” amesema.

Mzee Arfi aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara, sasa ni kada wa CCM.

Anasema uamuzi wa wajumbe wa Mkutano Mkuu umekiepusha chama na dhahama ambazo zingeweza kukikumba.

“Wangesema wasubirisubiri kidogo, kungeweza kuibuka makundi ya wanaotaka kugombea urais ndani ya CCM na kukivuruga chama.

“Hapa ninawapongeza sana wajumbe. Samia (Rais) anavyo vitu vya kuonyesha kuwa anafaa kuendelea kuliongoza taifa. Mfano, miradi ya kimkakati kama SGR (reli ya kisasa) na JNHPP (Bwawa la Umeme la Julius Nyerere). Alipoingia madarakani miradi hii ilikuwa chini ya asilimia 30, lakini sasa inafanya kazi,” amesema.

Kingine kikubwa kinachombeba Rais Samia, kwa mujibu wa Arfi, ni diplomasia ya kimataifa iliyokuwa imekufa kabisa kipindi cha nyuma.

Ameonyesha kufurahishwa na uteuzi wa Balozi Nchimbi kuwa mgombea mwenza akisema bado ana nguvu kuliko wanasiasa wengi kwa sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Dk. Rose Ruben, amesema Rais Samia anafaa kuchaguliwa kugombea nafasi ya Urais kupitia CCM kwa sababu kipindi chote alichohudumu amefanya vizuri na kuonyesha uwezo mkubwa katika kuongoza.

Amesema kwa sasa watu wanaendelea kuishi vizuri na kufanya shughuli zao bila kusumbuliwa kutokana mazingira na utulivu uliopo hapa nchini.

“Kwa maoni yangu anafaa kupewa nafasi tena kwa sababu amethibitisha kwamba wanaweza na pia kama alivyowahi kusema mwenyewe Rais Samia kwamba uongozi upo kwenye moyo wa mtu na akili hauangalii kwamba ni mwanamke au mwanaume,” anasema.

Kwa upande wake, mwanaharakati Ichikael Maro, anasema Rais Samia anafaa kwa kila kitu kwa sababu ameonyesha ni mwanamke kiongozi kwa muda wote aliohudumu.

Anasema katika kipindi chote cha uongozi wake ameonyesha uwezo wake kwamba wanawake wanaweza na ‘ametufanya tuheshimike’ hata kimataifa na sasa Tanzania inang’ara.

“Ushauri wangu aangalie namna ya kuwapangua mawaziri waliopo madarakani, kama itatokea amefanya kosa asihamishwe, badala yake aondolewe kabisa wengine wachukue nafasi kwa sababu wapo wenye uwezo nje wanahitaji nafasi,” amesema.

Mwenyekiti wa Wazazi Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, Pius Buzumale, anasema kazi aliyoifanya Rais Samia ndani na nje ya nchi inambeba na kumpambanua miongoni mwa wanasiasa wengi nchini.

“Hakuna ubishi, anafaa kugombea tena na kumalizia kipindi cha pili kilichobaki,” anasema Buzumale.

Wasifu wa Dk. Samia Suluhu Hassan:

Rais Samia Suluhu Hassan alizaliwa Januari 27, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.

Ameolewa na Hafidh Ameir na wamejaaliwa kupata watoto wanne; watatu wa kiume na mmoja wa kike.

ELIMU NA MAFUNZO

Dk. Samia alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chwaka, Unguja (1966 hadi 1968), Shule ya Msingi Ziwani (1970) na Shule ya Msingi Mahonda (1972).

Elimu ya sekondari aliipata katika shule za Sekondari Ng’ambo na Lumumba (1973 hadi 1976).

Mwaka 1983 alipata Astashahada katika Mafunzo ya Takwimu kutoka Chuo cha Uchumi, Zanzibar na kufanya kazi kwa kipindi kifupi Wizara ya Mipango na Maendeleo.

Mwaka 1983 hadi 1986 alijiunga na Chuo cha Maendeleo ya Uongozi Mzumbe (IDM) kusomea Utawala wa Umma.

Dk. Samia alipata mafunzo mbalimbali katika Chuo cha Utawala wa Umma, Lahore nchini Pakistan (1987); Eastern and Southern African Management Institute (ESAMI) (1991) na Taasisi ya Uongozi ya Hyderabad, India (1998).

Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza kwa ajili ya masomo ya juu ya uchumi. Alipata Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire, Marekani.

UZOEFU SERIKALINI

Dk. Samia ni Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aliapishwa kuwa Rais Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha Rais wa Tano, Dk. John Magufuli, hivyo kuwa mwanamke wa kwanza nchini kushika nafasi hiyo; baada ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais. 

Nyadhifa nyingine alizowahi kuzishika ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais; Muungano (2010-2015); Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji Zanzibar (2005-2010) na Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake na Watoto (2000-2005).

Mwaka 2014 alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba. Amewahi pia kuwa Afisa Mipango Rasilimali Watu (1987-1988) na Karani Masijala (1977-1983).

UZOEFU NDANI YA CCM

Dk. Samia alijiunga CCM Juni 10, 1987 kama mwanachama kabla ya kugombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi (Viti Maalumu) mwaka 2000.

Alidumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 2010 alipogombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Jimbo la Makunduchi, Zanzibar.

Mwaka 2002, alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, nyadhifa ambazo amedumu nazo hadi sasa.

UZOEFU KATIKA TAASISI NYINGINE

Mwaka 2016, Samia aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kuwa Mjumbe wa Jopo la UN kuhusu Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi; Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika hadi mwaka 2017.

Katika kipindi hicho aliwasilisha mambo 27 yaliyobainishwa na Serikali ya Tanzania kama hatua za kimkakati kuweka mfumo endelevu wa kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.

Pia Dk. Samia amefanya kazi na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) mwaka 1988 hadi 1997;

Amefanya kazi katika kamati, bodi na taasisi mbalimbali kama Parole ya Zanzibar (2001- 2010), Mlezi wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanzibar (1997-2000), Mjumbe Bodi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote – EOTF (1996-2000), Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Taasisi zisizo za Kiserikali Zanzibar (ANGOZA) 1995-2000, Mwanachama wa Lions Club Zanzibar (1991-1998), Mjumbe wa Kamati ya Uundaji wa Sera ya Elimu Zanzibar (1996) na Mwanachama Mwanzilishi wa Taasisi ya Kuchochea Maendeleo ya Wanawake Zanzibar (1991-1994).

Wasifu wa Balozi Nchimbi:

Dk. Emmanuel Nchimbi amezaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya. Elimu yake ya Msingi alianzia jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 hadi 1986.

Baba yake mzazi, Mzee John Nchimbi ni askari polisi aliyestaafu na cheo cha Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) akiwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara.

Mzee Nchimbi pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa vipindi viwili kupitia kundi la majeshi na baadaye Katibu wa CCM wa Mkoa, alikoma kushiriki masuala ya kisiasa mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa.

Dk. Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Uru Seminary kati ya mwaka 1987 hadi 1989 (kidato cha I–III) kisha akahamia Shule ya Sekondari Sangu na , kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990.

Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997).

Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuata (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).

Dk. Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003.

Alisoma Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara ya Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea katika maeneo ya benki na fedha.

Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda mwaka 2003–2005 na mwaka 2008–2011 alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Amemuoa Jane na wana watoto watatu.

Mbio za ubunge

Alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM. Ilipotimu mwaka 2005, aliingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu.

Dk Nchimbi alisaidiwa na mtandao mkubwa wa CCM na kupata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.

Baada ya kuwa mbunge, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, hii ilikuwa Januari, 2006, alidumu katika wizara hiyo hadi Oktoba, 2006 alipohamishiwa Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana – hapa pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba, 2006 hadi Februari, 2008 kisha Wizara ya Ulinzi na Jeshi Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba, 2010.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Nchimbi alijitosa tena Jimbo la Songea Mjini. Kampeni za 2010 zilimnyima usingizi pamoja na kuwa chama chake kilikuwa kimechukua asilimia zaidi ya 90 ya vijiji, vitongoji na mitaa mwaka 2009.

Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa Chadema na kumshinda kwa mara ya pili, japo safari hii akipoteza takriban ushindi wa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, alipata asilimia 59.9 dhidi ya 37.48 za Mbogoro.

Upandaji vyeo wa Nchimbi uliendelea, Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei, 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba, 2013.

Mwaka 2016, Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, akamteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil na alihudumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 2021 kisha mwaka 2022 aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri kisha Januari 15, 2024 akateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nafasi hiyo ya ukatibu mkuu anaendelea kuishikilia hadi sasa.

PHILLIP MPANGO NI NANI?

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, alizaliwa Julai 14, 1957 katika Kijiji cha Kasumo, Kasulu mkoani Kigoma, Kijiji ambacho pia alizaliwa baba yake, Isidori Mpango.

Dk. Mpango ni kaka mdogo wa Askofu (mstaafu) wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanganyika Magharibi – Kasulu, Dk. Gerard Mpango.

Ni mchumi mwenye shahada ya uzamivu. Kuanzia miaka ya 1990 hadi 2000, alifanya kazi akiwa Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi katika Kitivo cha Biashara (sasa Shule ya Biashara) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Pia amewahi kuwa Mchumi Mwandamizi wa Benki ya Dunia (WB), Mkuu wa Kamati ya kumshauri Rais wa Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete, kuhusu masuala ya uchumi na Katibu Binafsi wa Rais anayeshughulikia masuala ya uchumi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi, kabla ya kuhamishiwa Tume ya Mipango, Ofisi ya Rais.

Rais wa Tano, Dk. John Magufuli, alimteua kuwa Kaimu Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baada ya siku chache akateuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Katika uchaguzi wa mwaka 2020 alishinda ubunge Jimbo la Buhigwe kisha akateuliwa tena kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Machi 30, 2021 baada ya kifo cha Magufuli, Rais Samia Suluhu Hassan, akamteua Dk. Mpango kuwa Makamu wa Rais. MWIS