Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kilimanjaro

MKOA wa Kilimanjaro umeingia kwenye ukurasa mpya wa upatikanaji wa haki kwa uzinduzi rasmi wa Kliniki ya Sheria bila malipo, uliofanywa na Mkuu wa Mkoa, Nurdin Babu.

Hafla hiyo ilifanyika leo Januari 21, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wawakilishi wa taasisi za kisheria.

Kliniki hiyo ni sehemu ya juhudi za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Kilimanjaro, kuhakikisha huduma za kisheria zinawafikia wananchi moja kwa moja. Huduma hizi zitapatikana kuanzia Januari 21 hadi Januari 27, 2025, katika Viwanja vya Stendi ya Vumbi karibu na Stendi Kuu ya Mabasi Moshi.

Akihutubia wananchi na wadau waliohudhuria hafla hiyo, Babu ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa juhudi zake za kuimarisha utawala wa sheria nchini. Alisisitiza umuhimu wa wananchi wa Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi ili kupata msaada wa kisheria unaohitajika.

“Huduma hizi ni fursa adimu kwa wananchi kupata suluhisho la changamoto mbalimbali za kisheria bila gharama yoyote. Tunawashukuru sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana nasi kuimarisha haki na utawala wa sheria,” amesema Babu.

Aliendelea kueleza kuwa Kliniki hiyo itachangia kupunguza migogoro kati ya wananchi na serikali, sambamba na kuwaunganisha wananchi na mawakili wa serikali kwa ajili ya usuluhishi wa changamoto za kisheria.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Tamari Mndeme, amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake.

“Tunayo timu ya wataalamu wa sheria waliobobea ambao wapo tayari kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi. Tunatarajia kliniki hii kuwa jukwaa la kutatua changamoto nyingi zinazowakabili wananchi,” amesema Tamari.

Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wanahimizwa kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hii kuwasilisha matatizo yao ya kisheria, kama vile migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, na masuala mengine yanayohitaji msaada wa kisheria.

Uzinduzi huu ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha kila mwananchi anapata haki kwa wakati, huku ikisisitiza kuwa sheria ni msingi wa maendeleo ya jamii yoyote.