Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili Fredy Rajab Chaula na Bashiru Richard Chaula kwa tuhuma za kula njama ya mauaji ya Regina Rajab Chaula (62) mkazi wa Bahari Beach Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambaye ana makazi mengine nchini Denmark.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake mapema leo Januari 20, 2025, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne Muliro amesema mauaji hayo yametokea wakati mama huyo akiwa kwenye harakati za kufuatilia kesi zake za madai dhidi ya watuhumiwa hao, ambazo ziko Mahakama Kuu Divisheni ya haki jijini Dar es Salaam.
Mwili wa mama huyo ambaye alipotea katika mazingira ya kutatanisha tangu Desemba 13, 2024, umepatikana Januari 18, 2025, majira ya saa 8 mchana ndani ya nyumba yake.
“Wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa kupotea kwa mama huyo, lilibaini na kutilia mashaka shimo kubwa la maji machafu lililojengewa katika nyumba yake, ambapo lililazimika kulibomoa na kuukuta mwili wa marehemu”
Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi linalaani vikali kitendo hiko kibaya na cha kinyama alichofanyiwa mama huyo, na litahakikisha kila aliyekula njama ama kushiriki kwa namna yoyote anakamatwa na kufikishwa kwenye mamlaka za kisheria.