TikTok imerejesha huduma zake kwa watumiaji wake milioni 170 nchini Marekani baada ya Rais Mteule Donald Trump kusema atatoa agizo la kuipa programu hiyo ahueni atakapoingia madarakani rasmi hii leo.

Jumamosi jioni, programu hiyo inayomilikiwa na Wachina ilisitisha huduma zake kwa watumiaji wa Marekani, baada ya sheria ya kuipiga marufuku kwa misingi ya usalama wa taifa kuanza kutekelezwa.

Trump, ambaye hapo awali aliunga mkono marufuku dhidi ya jukwaa hilo, aliahidi Jumapili kusitisha kwa muda utekelezaji wa sheria hiyo ili kutoa nafasi ya majadiliano.

Baadaye TikTok ikasema kwamba ipo katika mchakato wa “kurejesha huduma”.

Muda mfupi baadaye, programu ilianza kufanya kazi tena. Watumiaji wake wa mtandao huo maarufu walimshukuru Trump kwa hatua hiyo.

Katika taarifa, kampuni hiyo ilimshukuru rais huyo mteule kwa “kutoa uhakikisho unaohitajika” na kuongeza kuwa itafanya kazi na Trump “kutafuta suluhisho la kudumu ambalo litaisaidia TikTok kuendelea na shughuli zake nchini Marekani”.