Donald Trump ameahidi kuchukua hatua kadhaa za kuzuia kile alichokiita “kuanguka kwa Marekani” mara tu atakapoapishwa rasmi kama rais wa nchi hiyo Jumatatu.
Akiwahutubia wafuasi wake walioujaza uwanja wa michezo wa One Sports Arena huko Washington usiku wa kuamkia Jumatatu katika mkutano wa kusherehekea ushindi wake, Trump amesema atakabiliana na wahamiaji.
“Tutasitisha kuvamiwa kwa mipaka yetu,” alisema Trump.
Trump hususan amewataja wahalifu kama sehemu ya wimbijipya la wahamiaji kutoka Venezuela. Ameahidi kuwaondoa nchini Marekani wanachama wa genge la Venezuela la Tren de Aragua.
Wafuasi wa Trump mjini Washington Wafuasi wa Trump mjini Washington
Wafuasi wa Trump mjini WashingtonPicha: Celal Gunes/Anadolu/picture alliance
“Hawa ni watu wabaya na wataondoka nchini mwetu,” rais huyo mteule alisema.
Sehemu kubwa ya hotuba ya saa moja nzima ya Trump imejikita katika uhamiaji, akisisitiza hoja ambayo ilimpelekea kupata ushindi mkubwa dhidi ya mpinzani wake Kamala Harris katika uchguzi wa mwezi Novemba.
Ni ipi mipango ya Trump ya siku ya kwanza?
Trump ameahidi kusuluhisha “kila tatizo” linaloikabili Marekani na kuweka amri kadhaa mpya katika siku zake za kwanza za urais wake.
“Katika historia ya Marekani, tutakuwa na siku bora zaidi ya kwanza ya urais, wiki bora zaidi ya kwanza na siku bora zaidi 100 za kwanza kuwahi kushuhudiwa,” alisema Trump.
Rais huyo mteule alisema atazitoa “rekodi zilizosalia kuhusiana na mauaji” ya Rais wa zamani wa Marekani John F. Kennedy, Seneta Robert Kennedy na mwanaharakati wa haki za kiraia Martin Luther King Jr.
Kabla kuingia madarakani mwaka 2017, Trump alitoa ahadi sawa na hizo ila akaishia kutoa nyaraka kadhaa tu za siri zinazohusiana na mauaji hayo.