Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ameilaani jamii ya kimataifa inayokosoa demokrasia nchini Rwanda, akisema inashindwa kuelewa ukweli wa hali halisi.
Akizungumza kuhusu mzozo unaoendelea kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda, Rais Kagame ameonyesha wasiwasi kuhusu shutuma zinazotolewa dhidi ya Rwanda, huku akitaja masuala ya usalama, siasa za maziwa makuu, na mizozo ya kanda hiyo yakiendelea kusumbua.
Rais Kagame alisema anashangaa kuona Umoja wa Mataifa ukikubaliana na serikali ya Congo kuhusu tuhuma kwamba Rwanda inashirikiana na kundi la M23, ambalo linadai udhibiti wa maeneo mengi ya mashariki mwa DRC
Alisema: “Nashangaa juhudi za kutatua mzozo zimefikia wapi”.
“ Ushahidi uliokuwepo haupewi uzito kianchopewa uzito ni kile ambacho amekisema mtu mwingine, hata kama hakina ukweli.”
Rais Kagame aliongeza kuwa Rwanda inalaumiwa kwa sababu jamii zinazozungumza Kinyarwanda mashariki mwa Congo zina uhusiano wa kihistoria na Rwanda, tangu enzi za ukoloni ambapo mipaka ya mataifa ilichorwa.
Aliishutumu jamii ya kimataifa kwa kushindwa kutatua mzozo huo kwa zaidi ya miaka 30, licha ya kujua wazi mzizi wa tatizo.
Amesisitiza kuwa lawama dhidi ya Rwanda hazitasaidia kutatua mzozo huu, na kuonya kwamba bila kutatua chanzo cha tatizo, hali ya mashariki mwa DRC itaendelea kuwa mbaya.
“Kama unadhani Rwanda iko mashariki mwa DRC kusababisha matatizo, jiulize kwa nini Rwanda imeamua kupigana pale,” alisema Rais Kagame
“Tutateseka vya kutosha, hatuwezi kamwe kurudi kule tulipotoka, haijalishi ukubwa wa watesi wetu.”
Mzozo huu umesababisha uhusiano wa Rwanda na Congo kuharibika vibaya, huku Rais wa DRC, Felix Tshisekedi, akiendelea kutishia mara kadhaa kushambulia Rwanda na kuondoa utawala wa Kigali.
Hata hivyo, Rais Kagame amemjibu Tshisekesi, akisema: “Mtu anayesababisha matatizo katika mzozo huu ni Tshisekedi, ambaye hajachaguliwa, na hiyo ni jambo mnalijua.”
Ripoti ya jopo la watafiti wa Umoja wa Mataifa imeitaja Serikali ya Kinshasa kwa kuwasaidia wanamgambo wa FDLR, kundi la waasi la kihutu, ambalo limeshatangaza vita dhidi ya Rwanda.
Hali hii, pamoja na Serikali ya Kinshasa kukataa kufanya mazungumzo na kundi la M23, inaendelea kutatiza juhudi za kumaliza mzozo wa mashariki mwa DRC.