Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
SERIKALI katika mwaka huu wa fedha 2025/2026 imetenga bajeti kubwa ya ununuzi wa vitabu vya ndani kama mkakati wa kuhamasisha waandishi na wachapishaji wa vitabu katika kukuza maarifa.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Profesa Rwekaza Mukandala, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wachapishaji na waandishi wa vitabu.
Mkutano huo wa siku mbili wa wachapishaji na waandishi wa vitabu uliandaliwa na bodi ya huduma za maktaba Tanzania na kufanyika kwenye ofisi za Maktaba Kuu ya Taifa jijini Dar es Salaam.
Alitaja mada mbili zilizojadiliwa kuwa ni utekelezaji wa sheria ya legal deposit kwenye maktaba mtandao jumuishi ya taifa na umuhimu wa ununuzi wa vitabu kwaajili ya ukuzaji wa soko la ndani.
Alisema bajeti hiyo kubwa inaonyesha namna ambavyo serikali imedhamiria kuunga mkono waandishi na wachapishaji wa ndani kwa kununua vitabu vingi vya ndani vyenye maudhui ya kitanzania kwaajili ya kurithisa utamaduni wa kitanzania.
“Kwa kuweka bajeti kubwa ya ununuzi wa vitabu vya ndani katika mwaka huu wa fedha tunatarajia itaongeza hamasa kwa waandishi na wachapishaji wengi wa Tanzania kushriki katika mchakato wa kukuza maarifa na elimu,” alisema na kuongeza
“Nawahimiza washiriki kutumia mkutano huu kama jukwaa la kujadili fursa zinazotokana na utekelezaji wa sheria ya amana na mchakato wa ununuzi wa vitabu itakayotolewa na watoa mada, mawazo yenu ni muhimu kuboresha kazi zetu na kuinua soko la vitabu hapa nchini,” alisema Mukandala.
Alisema serikali itaendelea kuhifadhi machapisho ya vitabu vya ajili ya kukuza maarifa na elimu kupitia vitabu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Profesa Mukandala alisema Sheria ya amana ya mwaka 1975 inasisiza umuhimu machapisho yote yanayochapishwa ndani ya nchi kuhifadhiwa kwenye maktaba kuu ya taifa ili kulinda na kuhifadhi urithi wa kitamaduni na kiakili kwaajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Alisema TLSB inatoa jukwaa la kidijitali ambalo linarahisisha uhifadhi, upatikanaji na usambazaji wa machapisho hayo kwa watumiaji wa ndani na nje ya nchi.
“Hii ni fursa kubwa kwa waandishi na wachapishaji wa vitabu katika kuweka hazina ya maarifa na kutambulisha kazi za ndani kimataifa na katika hilo tunapenda kusisitia ushirikiano wa karibu kati ya TLSB na wadau ili kuhakikisha machapisho yenu yanawafikia wadau wengi,” alisema
Alisema TLSB itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali nchini katika utekelezaji wa sheria ya amana ili kuwezesha fani kuwa nguzo muhimu ya maendeleo hasa katika kusukuma maendeleo ya taifa kwa kutumia maktaba jumuishi mtandaoni katika kukuza uchumi wa kidijitali.
“Maktaba jumuishi kitaifa mtandaoni inakwenda kuruhusu upatikanaji wa vitabu vingi kidijitali na usajili wa vitabu utafanyika mtandaoni kwa hiyo mfumo utarahisisha usambazaji wa vitabu na utasaidia soko la ndani na kukuza uchumi kupitia mabadiliko makubwa ya teknolojia,” alisema