Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Godbless Lema, amejitokeza hadharani kutoa ufafanuzi kuhusu tuhuma dhidi yake zilizotolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje kuhusiana na fedha zilizokusanywa kwenye kampeni ya ‘Join the Chain’.
Lema amesema licha ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kulitolea majibu suala hilo, lakini bado majibu yake hayakusafisha jina lake, kwani alitakiwa kusema hadharani kwamba Wenje ni muongo.
“Mchakato wa ‘Join the chain’ ulianza baada ya msajili wa vyama vya siasa kutishia kukifuta chama chetu kwa sababu hatukufanya mkutano wa Baraza Kuu kama sheria ya vyama vya siasa inavyotaka, na kwa wakati huo mwenyekiti wetu Freeman Mbowe alikuwa jela, hivyo Katibu Mkuu, John Mnyika akaitisha kikao kidigitali na kamati kuu cha kujadili hatma yetu”
Katika kikao hicho Katibu Mkuu alitaka kila mjumbe wa kamati kuu atafute kampuni au mdau wa kumpa pesa, jambo ambalo Lema alilipinga na kuleta wazo la kushirikisha wanachama wa CHADEMA duniani ili wachangie fedha kwa ajili ya chama chao, wazo lililokubaliwa na akateuliwa kuwa kiongozi wa mchakato huo.
Lema ameongeza kuwa mchakato huo ulipoanza alimwambia Katibu Mkuu afungue akaunti za chama ili michango yote ipitie huko na si kwenye akaunti zake binafsi, ambapo pia walikusanya fedha za kutengeneza magari ya chama yatakayowawezesha viongozi waliopo Tanzania kuzunguka kuhamasisha wanachama.
Aidha Lema amesema mchakato huo ulienda mbali zaidi kwa kuchangisha fedha nyingine za kumsaidia Mwenyekiti Mbowe kutoka gerezani kwa kumuwekea mawakili, sambamba na kuweka presha kwa serikali ili waweze kumfutia kesi ya ugaidi iliyokuwa ikimkabili.