SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Mitaji na Uwekezaji (UNCDF Tanzania) kwa kushirikiana na wadau wa Nishati Safi limetaka kuendelea kutolewa elimu ya matumizi ya nishati safi kwa jamii, ili kupunguza athari mbalimbali ikiwemo ukataji miti unaosababisha uharibifu wa mazingira.

Katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam wa kuangalia mwenendo wa soko la bidhaa za nishati safi ili kuchochea matumizi ya nishati safi zaidi nchini, wadau hao wamesema kuna umuhimu wa jamii kupewa elimu zaidi ili kuachana na matumizi ya mkaa na kuni yanayosababisha ukataji miti kwa ajili ya matumizi ya mkaa na kulinda afya hasa za wanawake wanaotumia muda mwingi jikoni kuandaa chakula kwa ajili ya familia.

Utafiti wa kimasoko uliowasilishwa katika mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana umeonesha pamoja na mambo mengine, mkaa ndio unaotumika zaidi katika matumizi ya kupikia na kuleta madhara mbalimbali ya kiafya, kusababisha ukataji miti ovyo na kuharibu mazingira. Pia utafiti huo umeonesha kuwa asilimia 50 ya mkaa unaozalishwa nchini unatumika katika mkoa wa Dar es Salaam.

Akiwasilisha mada kwenye mkutano huo, Meneja wa UNCDF Tanzania , Imanuel Muro amesifu jitihada zinazoendelea kati ya Serikali pamoja na wadau katika kuhamasisha jamii matumizi ya nishati safi ili kujiletea maendeleo.

Amesema mpango uliopo kwa taasisi yake ni kutumia wadau mbalimbali wakiwemo watu mashuhuri kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi.

Muro amesema UNCDF inaungana na wadau wengine ikiwemo Jumuiya ya Ulaya (EU) katika kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.

Muro amesema matumizi ya mkaa yamekuwa makubwa zaidi Tanzania kuliko kuni, na mkaa ni matokeo ya kukata na kuchoma misitu.

Naye Profesa Innocent Pantaleo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyetoa wasilisho la utafiti wa masoko kwa niaba ya Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa amesema matumizi ya nishati safi yatasaidia kuokoa misitu kwa kuwa matumizi ya kuni ni kichocheo cha uharibifu wa misitu na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi.

Akiwasilisha mada yake kwa wadau wa Nishati safi, Profesa Pantaleo amesema suala la Nishati Safi ni pana hivyo kuna kila sababu ya kutengeneza kategoria mbalimbali likianzia suala la umuhimu wake.

Amesema umuhimu wa matumizi ya nishati safi ni kuokoa mazingira lakini pia ametaka mpango huo uwe nafuu ili kila jamii ya Watanzania imuudu gharama.

Mkutano huo ni mfululizo wa mikutano mbalimbali iliyofanyika kwa kuwaleta pamoja Serikali, wadau na wafanyabishara wa bidhaa zinazochochea matumizi ya nishati safi ili kuangalia namna ya kuisaidia jamii kutumia nishati safi mbadala badala ya mkaa na kuni.

UNCDF kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika mkutano uliofanyika mwaka jana waliiomba Serikali kutunga sera ili kuwabana wanaoingiza vifaa visivyo na ubora kwa kisingizio cha mpango huo.

Mkutano huo umeandaliwa na UNCDF na umefadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO), UNCDF, Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) na CoockFund.