Rais mteule wa Marekani Donald Trump atatafuta njia ya kuzuia kufungwa kwa TikTok kabla ya marufuku dhidi ya programu hiyo kuanza kutekelezwa wikendi hii, mshauri wake ajaye kuhusu usalama wa taifa amesema.

Mbunge Mike Waltz wa Florida, alisema Trump ataingilia kati iwapo Mahakama ya Juu Zaidi itaendeleza sheria inayopiga marufuku jukwaa hilo nchini Marekani isipokuwa iuzwe ifikapo tarehe 19 Januari.

Katika wiki yake ya mwisho, utawala wa Biden pia unatafuta njia za kuzuia TikTok kutoweka ghafla, inaripoti NBC News.

Mmiliki wa Uchina ByteDance amesema inapanga kuzima programu hiyo kwa watumiaji wake milioni 170 wa Marekani ifikapo Jumapili.

“Tutachukua hatua stahiki ili kuzuia TikTok isifungwe,” Waltz alisema Alhamisi.

Alibainisha kuwa sheria inaruhusu kuongezwa kwa siku 90 kwa ByteDance ikiwa hatua kubwa imefanywa kuelekea kuuzwa.

“Kimsingi hilo litakuwa linampa Rais Trump muda ili TikTok iendelee kufanya kazi,” Waltz alisema.

Siku moja kabla, mshauri wa usalama wa kitaifa anayeingia alidokeza kwenye Fox News kwamba Trump alikuwa akipanga kutoa amri yake katika juhudi za kuzuia marufuku hiyo.

Hata hivyo, haijulikani ikiwa hatua kama hiyo inaweza kukwepa sheria iliyopitishwa na Congress.

Programu hiyo imepigwa marufuku kwa misingi ya usalama wa taifa, kwa sababu ya wasiwasi kwamba data iliyonayo inaweza kukusanywa na Chama cha Kikomunisti cha China.

Lakini kwa mujibu wa gazeti la New York Times, Trump amemwalika mtendaji mkuu wa TikTok, Shou Zi Chew, kuhudhuria kuapishwa kwake urais Jumatatu ijayo, akipewa nafasi ya wageni waheshimiwa kwenye jukwaa.