Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imewataka wale wote ambao hawakujitokeza kuchukua vitambulisho vyao vya Taifa vilivyopelekwa katika ofisi za Kata, Vijiji, Mitaa, Vitongoji na Shehia kufika katika ofisi za NIDA za wilaya walikojisajili kuchukua vitambulisho vyao mara watakapopokea ujumbe mfupi wa maandishi katika simu zao za mkononi (sms) unaowataka kufanya hivyo Atakayeshindwa kufanya hivyo matumizi ya Namba yake ya Utambulisho wake wa Taifa (NIN) yatasitishwa baada ya mwezi mmoja tangu kupokea ujumbe huo.
Hatua hiyo imechukuliwa ili kuhakikisha vitambulisho vyote vilivyozalishwa na kupelekwa katika ofisi za za Kata, Vijiji, Mitaa, Vitongoji na Shehia ili wananchi waweze kuvichukua huko kwa vinachukuliwa na wahusika. Awali NIDA baada ya mwezi Oktoba 2023 mpaka Machi 2025 kuendesha zoezi maalum la kuzalisha vitambulisho kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya wananchi wengi waliokuwa na Namba za Utambulisho wa Taifa pekee kwa muda mrefu, ilivipeleka vitambulisho hivyo kwenye ofisi za Kata, Vijiji, Mitaa, Vitongoji na Shehia ili kuondoa usumbufu wa wananchi kuchukua vitambulisho hivyo badala ya kuvifuata katika ofisi za NIDA za Wilaya.
“Tulipeleka vitambulisho vingi sana chini kwa wananchi katika ofisi za Vijiji na Mitaa yao ili kuwarahishia wananchi kupata vitambulisho hivyo lakini bado kuna vitambulisho havijachukuliwa na wahusika hivyo tumevikusanya vyote na kuvirejesha katika ofisi za NIDA za wilaya” amesema Geofrey Tengeneza Mkuu wa KItengo cha Mawasiliano cha NIDA.
Amesema Mamlaka imekamilisha zoezi la kukusanya vitambulisho vyote kutoka ofisi hizo za Kata, Vijiji na Mitaa na kuvirejesha katika ofisi za NIDA katika Wilaya zote nchini na tayari ujumbe mfupi wa simu za mkononi (sms) zimeanza kutumwa na wameanza kujitokeza kuchukua vitambulisho vyao. Ameongeza kuwa hatua hii ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Mambo yaNdani ya Nchi Mhe. Innocent Bashungwa aliyoyatoa kwa Mamlaka hiyo kuhakikisha vitambulisho vyote ambavyo havijachukuliwa va wahusika vinachukuliwa ndani ya miezi miwili.