Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imetoa elimu  kwa viongozi wa serikali za mitaa Kariakoo, kuhusu sheria mbali mbali za ulipaji kodi ikiwamo kodi ya zuio la pango, namna  mpangaji wa nyumba anavyopaswa kukata sehemu ya kodi ya mwenye nyumba na kuilipa TRA.

Elimu hiyo imetolewa leo Januari 16, 2024 jijini Dar es Salaam na Afisa Mwandamizi wa kodi Mkoa wa Kikodi Kariakoo, Mashenene Beni wakati wa semina ya siku moja kwa viongozi hao wa serikali za mitaa kuhusu sheria za pango za nyumba.

Meneja wa TRA Mkoa wa Kodi wa Kariakoo, Kabula Mwemezi (aliyesimama)  akizungumza katika wa semina ya siku moja kwa viongozi wa Serikali za mtaa mkoa wa kodi Kariakoo ambapo pamoja na mambo mengine viongozi hao wamepewa elimu ya ukusanyaji wa kodi za pango katika nyumba za biashara na makazi.

Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Kodi, mpangaji wa nyumba anapaswa kumkata mwenye nyumba asilimia 10 ya kodi kabla ya kumlipa malipo yake.

Benny, amesema kodi hiyo kisheria inajulikana kama kodi ya zuio la pango ambalo baada ya kuikata kwa mwenye nyumba mpangaji anatakiwa kuipeleke TRA.

“Kodi ya zuio la pango ni kodi ambayo inapaswa ilipwe na mwenye nyumba, kwa sababu kisheria mpangaji anapomlipa mwenye nyumba anatakiwa azuie asilimia 10 ya malipo yake kwa mwenye nyumba huyo,”amesema Beni

“Kodi ya zuio la pango ni kodi ambayo inatokana na biashara ya kupangisha, kwa hiyo mwenye nyumba anapompangisha mtu, mpangaji anatakiwa azuie asilimia 10 ya malipo anayolipa kwa mwenye nyumba huyo kwa sababu kisheria inatakiwa ilipwe kwa Mamlaka ya Kodi TRA .”

Ameongeza kuwa, siyo nyumba ya kupanga kwa ajili ya kuishi pekee ndio inatakiwa kukatwa asilimia 10 ya zuio la pango, bali hata kwa yule anayepanga kwenye sehemu ya biashara.

Amefafanua kuwa, ikitokea labda mpangaji amepanga flemu ya duka kwa mwenye nyumba, na analipa Sh.milioni moja kwa mwezi halafu mkataba wao ni wa miezi mitatu, hivyo katika kiasi cha Sh.milioni tatu, anatakiwa kukata Sh.300,00 kama kodi ya zuio la pango akamlipa Sh. 270,000, 000 pekee na hiyo inayokatwa inapelekwa TRA.

Ameeleza kuwa tatizo kubwa linalochangia watu kushindwa kutekeleza hayo, ni kutokana na kutokujua sheria na kwamba wao kama TRA wataendelea kutoa elimu kuhusu kodi mbalimbali ili kila mtu atimize wajibu wake.

Pia, amesema eneo jingine ambalo bado kuna shida ya uelewa ni namna ya kulipa kodi inayotokana na uuzaji wa rdhi na kwamba kifungu cha 90(1) cha Sheria ya Kodi ya Mapato, kinaeleza kuwa, kama mtu anapata faida kwa kuuza ardhi au jengo lake, anatakiwa alipe asilimia 10 ya faida kama kodi.

“Hii italipwa kama kutakuwa na uthibitisho wa gharama za ujenzi, na gharama nyingine zinazohusiana na jengo na kama hakutokuwa na uthibitisho wa gharama, basi kodi itakuwa ni asilimia tatu ya thamani ya ardhi au jengo lililouzwa,”amesema Beni.

Amewataka viongozi wa mitaa kuhakikisha wanashirikiana na Mamlaka hiyo kutekeleza sheria hiyo ya kodi ya majengo na ardhi hususani wanaposhiriki katika upangaji au kwenye mauziano wa ardhi.