Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) imeitaka sekta binafsi Tanzania kutumia fursa ya maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam kuitumia fursa hiyo kufanya biashara na kuongeza mapato ya taifa kuinua uchumi wa nchi.

Akizungumza wakati wa ziara ya Umoja wa Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw Abed Gallus amesema maboresho yaliyofanywa yamekidhi vigezo, mahitaji na matarajio ya wafanyabishara na kuiweka bandari kwenye ushindaji wa kimataifa.

Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es salaam Bw. Abed Gallus (wakwanza kushoto) ambaye amemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mbossa akimkabidhi zawadi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Bw. Hamis Livembe walipotembelea bandari ya Dar es salaam kujionea uwekezaji uliofanyika katika bandari hiyoo.

Bw Gallus ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu TPA, Bw Plasduce Mbossa alisema uwekezaji mkubwa umefanywa kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye miundombinu kama eneo la upakuaji na upakiaji mizigo kwa kutumia vifaa vya kisasa, ambapo kazi hiyo kwa sasa inafanyika ndani ya muda mfupi tofauti na hapo awali.

“ Mashine za kupikia na kushusha mizigo yaani ‘Cranes’ zimerahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi mkubwa bandarini hapa. Ni nafasi ya pekee kwa sekta binafsi kuchangamkia,” alisema Gallus.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema TPA ina mpango wa kujenga bandari kavu (ICDs) katika eneo la Shimo la Udongo Kurasini jijini hapa kwa ajili ya kuhifadhia mizigo inayoharibika kwa haraka (perishable goods) kama vile matunda katika vyumba maalum vyenye ubaridi.

“Huko nyuma, mizigo ya bidhaa zinazowahi kuharibika ilikuwa inapitia katika bandari ya nchi jirani, lakini hivi sasa mizigo hiyo itakuwa inahifadhiwa katika bandari kavu ikisubiri kusafirishwa kwenda nje ya nchi,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es salaam Bw. Abed Gallus (aliyenyosha mkono katikati) ambaye amemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Bw. Plasduce Mbossa akitoa maelezo juu ya maboresho yaliyofanyika katika bandari ya Dar es salaam kwa ujumbe kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) walipotembelea katika bandari ya Dar es Salaam kujionea uwekezaji uliofanyika katika bandari hiyoo, watatu kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Bw.Hamis livembe, na wapili kushoto ni Meneja wa Mahusiano wa Kampuni ya DP world Tanzania Bw. Elitunu Mallamia.

“Kufuatia maboresho tuliyoyafanya, hivi sasa hakuna tena malalamiko ya kuchelewa kutolewa kwa mizigo inayowasili bandarini na badala yake, kutokana na kasi ya utendaji iliyopo, wateja ndio wanaochelewa kuja kuchukua mizigo yao,”

Alisema TPA ina maeneo makubwa ya kuhifadhi mizigo na kutoawito kwa wafanyabishara kuchukua mizigo yao kwa wakati bandarini kwani bandari siyo sehemu ya kuhifadhi mizigo kwani mizigo yote ya wateja inatakiwa itoke ili kutoa nafasi kwa mizigo mingine.

“Kasi ya ushushaji wa shehena itaboreka zaidi wateja watakapochukua mizigo yao kwa wakati,” amesema Gallus alisema na kuongeza kuwa TPA imejipanga na itaendelea kuwa lango imara la Uchumi.

Naye Meneja Mahusiano wa Kampuni ya DP World Tanzania, moja ya kampuni iliyowekeza katika bandari hiyo ya Dar es Salaam , Bw Elitunu Mallamia amesemakinachotokea sasa hivi katika bandari ya Dar es Salaam ni mizigo kusubiri wateja kuondolewa na siyo uchelewashaji tena kutokana na kasi ya utendaji iliyopo .

“Tumeweza kuhudumia shehena asilimia 25 zaidi kwenye miezi hii ambayo tumefanya kazi kuanzia mwezi Mei 2024 mpaka sasa Januari 2025),”Bw Mellamia alisema na kuongeza kuwa kwa mwezi Desemba pekee magari 25,251 yalishushwa kwenye meli 16 na kuvunja rekodi.

Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es salaam Bw. Abed Gallus (wanne kushoto) ambaye amemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mbossa akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) walipotembelea katika bandari ya Dar es salaam kujionea uwekezaji uliofanyika katika bandari hiyoo, watano kushoto ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara BW.Hamis livembe, na wakwanza kushoto ni Meneja wa Mahusiano wa Kampuni ya DP world Tanzania Bw. Elitunu Mallamia

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara, Bw Hamis Livembe aliipongeza TPA kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuleta mageuzi makubwa kwenye bandari zote hapa nchini.

“Miaka miwili iliyopita, tulikuwa na kilio cha ucheleweshwaji wa mizigo kutoka bandarini na wakati mwingine biashara zilichelewa kuwafikia wateja kwa wakati,” alisema nas kuongeza kuwa maboresho yaliyofanyika yameleta suluhisho la kudumu.