Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Timu ya Uchunguzi iliyoundwa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kuchunguza mali ya Msikiti wa Manyema, Kariakoo Jijini Dar es Salaam imebaini ubadhilifu na upotevu wa mali na fedha kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni mbili.
Akizungumza mara ya kukabidhiwa ya riporti iliyosheheni taarifa ya uchunguzi uliofanyika kufuatilia na kukagua mali na fedha baada ya kuwepo kwa malalamiko ya tuhuma za ubadhilifu zilizowasilishwa na baadhi ya waumini na viongozi wa msikiti huo jana, kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi alisema hatua stahiki za sheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika wote.
“‘Napenda kuutaarifu umma kwamba timu ya uchunguzi imekamilisha kazi yake na kubaini ubadhirifu wa fedha wa zaidi ya shilingi bilioni mbili, upotevu wa mali za taasisi ikiwemo viwanja na matumizi mabaya ya Madaraka na kuongeza kwamba wale wote wanaohusika watafikishwa katika vyombo vya uchunguzi kwa ajili ya hatua zaidi.,” amesema Bw Kanyusi.
Alisema Julai 09, 2024 aliitisha kikao kiliwajumuisha Makatibu wa BAKWATA kwa Wilaya ya Ilala na Mkoa wa Dar es Salaam, Bodi ya Wadhamini iliyovunjwa na baadhi ya wanachama wa Msikiti wa Manyema lengo likiwa ni kutafuta suluhu ya mgogoro wa Msikiti huo ambapo ilibainika uwepo na tuhuma za ubadhirifu wa mali za Msikiti.
“Nilitumia mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 14 cha Sheria ya Usajili wa Bodi za Wadhamini Sura ya 318 na kuunda Timu ya Uchunguzi kwa ajili ya kuchunguza tuhuma za ubadhirifu wa mali za Msikiti wa Manyema,” alisisitiza.
Bw Kanyusi alisema baadhi ya kazi ya timu hiyo ya Uchunguzi iliyotakiwa kuzifanya ni pamoja na kuhakiki na kujiridhisha na uhalali wa mali zote zinazomilikiwa na Msikiti wa Manyema sambamba na kupitia vyanzo vyote vya mapato ili kubaini kama mapato husika yanakusanywa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo.
Bw Kanyusi pia amezitaka Bodi za Wadhamini za taasisi zote zilizosajiliwa RITA zijikite katika kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika Katiba za taasisi zao na kuhakikisha zinasimamia na zinadhibiti ubadhirifu wa fedha na mali za taasisi ili kuepuka kuchukualiwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Baraza Kuu la Waislam BAKWATA Taifa, Bw. Rashid Salam alisema Baraza hilo litaendelea kushirikiana na RITA kufuatilia taasisi zote zilizopo chini yake ili kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao kwa kufuata katiba zao na sheria za nchi pamoja na kuwa waadilifu katika kusimamia mali za waumini wao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito ya msikiti wa manyema, Bw. Said Bakari Isihaka amesema kuwa kwa sasa waumini na baadhi ya viongozi wanasubiri taratibu za kisheria na maelekezo ya vyombo vya maamuzi ili kila mmoja aliyehusika na ubadhilifu wa mali na fedha aweze kuwajibika kwa kurudisha amana zote za msikiti na ikiwezekana wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma zao.
Naye, Mjumbe wa Kamati ya Mpito ya Msikiti wa Manyema, Bw Ismail Aden Rage amesikitishwa na vitendo vya ufisadi vilivyofanywa na baadhi ya viongozi hao na kutaka hatua za kisheria kuchukuliwa ili wahusika wote warudishe mali na fedha zilizopotea na kufikishwa mahakamani.