Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata askari wawili wa usalama barabarani walioonekana kwenye video iliyosambaa mitandaoni wakifanya vitendo visivyo na maadili vya kuchafua taswira ya Jeshi la Polisi.

Akizungumza na wanahabari leo Januari 15, 2025 Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema askari hao ambao ni Koplo John na WP Koplo Mgisi, kwa sasa wapo mahabusu na tayari hatua za kinidhamu za mashtaka ya kijeshi zimeanza, huku wakisubiria hatua nyingine za kisheria.

Video hiyo iliyosambaa mitandaoni inawaonesha askari hao wakichukua rushwa kwa madereva wa magari madogo na mabasi ya abiria.

Katika hatua nyingine Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vyovyote vya kulidhalilisha jeshi, vilivyo kinyume na maadili ya jeshi au kuchafua taswira ya Serikali.