KIZZA Besigye, mwanasiasa mkongwe wa upinzani na hasimu wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni, alitekwa nyara akiwa jijini Nairobi Novemba 2024 na kurejeshwa Uganda alikofunguliwa mashtaka katika mahakama ya kijeshi.
Kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, atafikishwa mahakamani kwa kosa zito la usaliti, mahakama ya kijeshi iliamua Jumanne, hatua inayoongeza changamoto za kisheria anazokabiliana nazo kabla ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwaka 2026. Kosa la usaliti lina adhabu ya kifo kwa wanaopatikana na hatia.
Besigye, ambaye amegombea urais mara nne, alitoweka jijini Nairobi, Kenya, Novemba 16. Siku chache baadaye, yeye na msaidizi wake, Obeid Lutale, walifikishwa mahakamani mbele ya mahakama ya kijeshi jijini Kampala, mji mkuu wa Uganda.
Besigye alishtakiwa kwa kumiliki silaha kinyume cha sheria na kwa tuhuma za kuomba msaada wa kijeshi kutoka nje kwa lengo la kuvuruga usalama wa taifa. Besigye, aliyekanusha mashtaka hayo, amewekwa rumande tangu wakati huo.
Mwendesha mashtaka wa kijeshi Jumatatu alibadilisha hati ya mashtaka na kuongeza shtaka la usaliti pamoja na kumtaja mshukiwa wa tatu, ambaye ni afisa wa jeshi, hatua iliyowashangaza mawakili wa utetezi waliopinga mabadiliko hayo.
Besigye, mwenye umri wa miaka 68, amekamatwa na kushambuliwa mara nyingi katika maisha yake ya kisiasa lakini hajawahi kupatikana na hatia ya uhalifu.