Ukraine imeshambulia maeneo kadhaa ya Urusi siku ya Jumanne katika kile inachosema ni shambulio lake “kubwa zaidi” hadi sasa.

Maghala ya kuhifadhia risasi na viwanda vya kemikali vilishambuliwa katika mikoa kadhaa, baadhi yao ikiwa mamia ya kilomita kutoka mpakani, kulingana na Mkuu wa Wafanyakazi wa Kikosi cha Wanajeshi cha Ukraine.

Vyanzo vya shirika la ujasusi la Ukraine SBU viliiambia BBC kwamba shambulio hilo la usiku lilikuwa “pigo kubwa” kwa uwezo wa Urusi katika vita.

Urusi ilisema kuwa imedungua makombora ya Atacms yanayotolewa na Marekani pamoja na makombora ya Uingereza ya Storm Shadow, na kuapa kujibu mashambulizi hayo.

Angalau viwanja tisa vya ndege katikati na magharibi mwa Urusi vilisimamisha shughuli zake kwa muda, huku mashambulizi hayo yakisababisha shule za kusini magharibi mwa mkoa wa Saratov kufungwa.

Mashambulizi katika eneo la mpakani la Bryansk yalisababisha milipuko katika kiwanda cha kusafisha mafuta, maghala ya risasi na kiwanda cha kemikali kinachosemekana kutengeneza baruti na vilipuzi, chanzo cha usalama cha Ukraine kiliiambia BBC.

Maafisa katika eneo la magharibi la Tula pia waliripoti shambulio la usiku mmoja, ambapo gavana wa eneo hilo Dmitry Milyaev alisema ulinzi wa anga umedungua ndege 16 zisizo na rubani.

Hakukuwa na majeruhi, alisema, ingawa vifusi vinavyoanguka vimeharibu baadhi ya magari na majengo.

Ukraine ilisema Urusi pia ilianzisha mashambulizi ya makumi ya ndege zisizo na rubani kote Ukraine usiku kucha, huku ving’ora vingi vya kutoa onyo vikisikika ndani na karibu na Kyiv.