Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt:Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya sheria kitaifa yanayotarajiwa kufanyika februari 3 katika viwanja vya chinangali mjini Dodoma.

Akitoa taarifa hiyo katika mkutano na wanahabari, Jaji mkuu Prof: Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa maadhimisho hayo ya wiki na siku ya sheria ni jukwaa linakowakutanisha mahakama na wadau to wake muhimu ili kutoa elimu ya shughuli zinazoendeshwa na mahakama.

“Maadhimisho ya wiki na siku ya sheria ni jukwaa maalum linakowakutanisha mahakama na wadau wake muhimu hususani wananchi ili kutoa elimu ya shughuli zinazotolewa na mahakama katika mnyororo wa utoaji haki”.

Aidha jaji mkuu ameongeza kwa kusema kuwa uzinduzi wa wiki ya sheria utaongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt: Jakaya Kikwete mjini Dodoma katika viwanja vya mwalimu Nyerere (Nyerere square) .

“Uzinduzi wa wiki ya sheria utafanyika januari 25 na utatanguliwa na mbio maalum (fun run) za kilomita 10 ambazo zitaambatana na matembezi ya umbali wa kilomita tano kwa wale ambao watapendelea kutembea katika hizo mbio maalum na matembezi ya tarehe 25 januari tutaongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt: Jakaya Kikwete”

Jaji mkuu amebainisha pia kuwa, maadhimisho ya wiki ya sheria na siku ya sheria yatafanyika katika ngazi ya kitaifa, kanda za mahakama kuu, divisheni za mahakama kuu, mkoa na wilaya zote nchini ambapo elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria itatolewa katika maeneo mbalimbali.