Na Mwadishi Wetu

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, amewahimiza wananchi wanaopata huduma katika mahakama mbalimbali nchini kutoa taarifa endapo hawajaridhishwa na huduma walizopewa.

Akizungumza leo Januari 14, 2025, katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Kifamilia kilichopo Temeke, Dar es Salaam, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria 2025, Profesa Juma alisisitiza umuhimu wa maoni na mrejesho kutoka kwa wananchi.

“Wananchi wanaweza kuripoti kwa kuandika maoni yao hata bila ya kutaja majina. Maoni hayo yatafika sehemu husika. Wengi wanakuwa na hofu wanapofika mahakamani, hata wasomi au wenye nyadhifa za juu. Hali hiyo ni ya kawaida kwa mtu yeyote anayefika mahali asipoyafahamu, lakini tunataka kuwaondolea uoga huo,” alisema Profesa Juma.

Profesa Juma alisema kuwa zipo njia mbalimbali za kutoa maoni na kuripoti changamoto zinazopatikana mahakamani, ikiwemo kupitia barua pepe za mahakama, simu moja kwa moja, tovuti ya Mahakama Kuu, au kuwasilisha moja kwa moja kwenye ofisi husika.

Aidha, kuelekea maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria, Profesa Juma alieleza kuwa Mahakama imejipanga kutoa elimu ya sheria kwa wananchi kwa kutumia magari maalum. Magari hayo yatawafuata wananchi katika maeneo yao ya kazi na kwenye shule kwa lengo la kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria.

“Tathmini tuliyofanya inaonyesha kuwa asilimia 40 ya wananchi hawafahamu shughuli za Mahakama na umuhimu wa Wiki ya Sheria. Mwaka huu, tumejipanga kuwafikia wananchi moja kwa moja ili kuwapa elimu hii muhimu,” aliongeza.

Katika hotuba yake, Profesa Juma aliipongeza Mahakama ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa ushirikiano mzuri, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia katika kuboresha huduma.

“Ni muhimu kuwa makini na mabadiliko ya teknolojia, hususan matumizi ya akili bandia (AI), ambayo yanaweza kuathiri ufanisi wa mahakama zetu. Teknolojia itumike vizuri ili kuondokana na changamoto zinazoweza kuitokeza,” alisisitiza.

Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria ni: “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”

Profesa Juma alihitimisha kwa kuwasihi wananchi kutoziogopa mahakama, akibainisha kuwa mahakama zipo kwa ajili ya kuwahudumia na kutatua changamoto zao mbalimbali.