Bunge la Lebanon limemchagua mkuu wa jeshi la nchi hiyo kuwa rais, na kumaliza ombwe la mamlaka lililodumu kwa zaidi ya miaka miwili.

Joseph Aoun uliungwa mkono na vyama kadhaa vya kisiasa, pamoja na Marekani, Ufaransa na Saudi Arabia.

Mpinzani anayeungwa mkono na wanamgambo wa Hezbollah alijiondoa siku ya Jumatano na kumuunga mkono kamanda huyo.

Urais ni jukumu lisilo la nguvu kisiasa ambalo hasa limetengwa kwa ajili ya Mkristo chini ya mfumo wa kugawana madaraka kupitia madhehebu.

Uchaguzi huo umefanyika wiki sita baada ya Lebanon kusitisha mapigano ili kumaliza vita vikali kati ya Israel na Hezbollah, ambavyo vilidhoofisha kwa kiasi kikubwa kundi hilo la Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaoungwa mkono na Iran.

Aoun, 60, ni mwanajeshi ambaye amekuwa kamanda wa jeshi tangu 2017.

Mgombea urais nchini Lebanon kwa kawaida anaweza kuchaguliwa katika duru ya kwanza ikiwa atapata theluthi mbili ya wengi – au kura 86 – katika bunge lenye viti 128, au kwa wingi wa kura katika duru ya pili.

Katika duru ya kwanza ya Alhamisi asubuhi, wabunge 71 walimpigia kura Aoun, 15 pungufu ya kile alichohitaji. Wabunge wengine 37 – wengi wao kutoka Hezbollah na Amal – hawakupiga kura, wakati kura 20 zilitangazwa kuwa batili.

Hatimaye, Aoun alichaguliwa kuwa rais baada ya kupata kura 99 katika duru ya pili, na hivyo kupata theluthi mbili ya kura zinazohitajika. Wabunge tisa hawakupiga kura, na kura 18 ziliharibika.