Na Magrethy Katengu, JamuhuriMedia, Dar es Salaam
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa kituo kikuu cha kushindilia gesi asilia (CNG) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam.
Ametangaza kuwa kituo hicho, kinachojengwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ambapo kitaanza kutoa huduma za kujaza gesi asilia kwenye magari kuanzia Februari 2025.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo Januari 9, 2025, Dk. Biteko amesema kukamilika kwa kituo hicho kutarahisisha upatikanaji wa gesi asilia kwa Watanzania, hususan wanaotumia nishati hiyo vyombo vya Moto ikiwemo magari, Pikipiki, bajaji .
“Serikali imeelekeza kujengwa kwa vituo vingine vya gesi asilia saba vya ziada na vituo hivyo vinajengwa na sekta binafsi imeahidi kuvijenga katika Mkoa wa Dar es Salaam, na tutaanzisha vituo vya kujaza gesi vinavyotembea—kimoja Morogoro na viwili Dodoma,” amesema Dk. Biteko.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amebainisha kuwa wamekubaliana na Shirika la Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuleta mabasi yanayotumia gesi asilia ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kupunguza utegemezi wa nishati chafu dizeli na Petroli.
Profesa William Anangisye, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambacho kimetoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiko amesema kituo kitatoa fursa kwa wanavyuo wanasoma masomo ya masuala ya gesi kwani kitaleta tija ya mafunzo kwa vitendo .
Mradi huu unaashiria hatua muhimu katika kuboresha upatikanaji wa nishati safi na rafiki kwa mazingira nchini Tanzania.