Na Mwandishi Wetu, Kibaha

WIZARA ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema jumla ya wilaya 108 nchini zimefikiwa na ujenzi wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa hatua ambayo imesaidia kurahisisha mawasiliano ya data hususani maeneo ya vijijini.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Meryprisca Mahundi amesema hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa katika Wilaya Chalinze na Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.

Amesema serikali kupitia Shirika la Mawasiliano (TTCL) wamefanikiwa kusambaza miundombinu ya mawasiliano katika wilaya 108 kati ya wilaya 139 zilizolegwa na kwamba wilaya 31 zilizobaki mwezi Julai mwaka huu zitakuwa zimefikiwa.

“Tunashukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha ambazo zimetuwezesha sisi ikiwemo shirika letu kufanya ujenzi wa miundombinu hii ya mawasiliano ambapo fedha hizi zimewezesha wilaya 108 kupata mawasiliano,”amesema Maryprisca.

Mhandisi Mahundi amesema lengo la serikali ni kuifanya Tanzania kuwa ya kidigtali na kufikia nchi zote za Afrika Mashariki na Jumuiya ya SADC na badaaye katika mabara mengine ikiwemo Asia na Ulaya.

“Tunaona namna tunavyoongeza wigo katika utoaji wa huduma mwanzo tulikuwa na uwezo kutoa jigabaiti 200 na mpaka sasa tunatoa kwa kiwango cha jelabaiti 2 kwa nchi nzima haya ni mafanikio mkubwa kwa serikali na shirika letu la (TTCL),” amesema.

Maryprisca aliuagiza uongozi wa TTCL kahakikisha ulinzi unaimafishwavyema katika vituo vyote vya mkongo wa taifa hatua ambayo itasaidia kukabiliana na hujuma dhidi ya Mkongo wa Taifa na serikali kwa ujumla.

Meneja wa TTCL Pwani, Randy Nyangusi amesema vituo vyote vya Mkongo wa Taifa katika Mkoa wa Pwani ulinzi umeimarishwa na kwamba jitihada mbalimbali kinaendelea kahakikisha vinaendelea kuwa salama.

“Mkongo huu wa taifa ni muhimu sana kwa nchi yetu hasa katika nyanja nzima ya uchumi kutokana na kitambua hilo tunaboresha usalama na ulinzi kila wakati katika miundombinu yote ya mawasiliano,” amesema Nyangusi..